June 24, 2021

RAIS AT APONDA KATIBA BMT

WAKATI sakata la sifa za kielimu la Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT), John Bayo likizidi kuchukua hatua tofauti, shirikisho limedai linatarajia kufanya mabadiliko ya katiba yake.


AT ilifanya uchaguzi wake mapema mwaka huu, baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya katiba, ambapo baadhi yake ni kipengele cha sifa ya kugombea kwa nafasi ya Rais na Makamu, kuwa na kiwango cha elimu ya kuanzia Diploma.


Lakini kuelekea uchaguzi na mara baada ya kufanyika, baadhi ya wadau wamekuwa wakiibuka na kudai Bayo hana sifa hiyo ya elimu.


Kwa nyakati tofauti, wadau hao wamefikia hatua ya kuandika barua hadi kwa Waziri mwenye dhamana na Michezo, Innocent Bashungwa, wakitaka katiba iheshimiwe.


Mbali na Waziri, pia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo, wamefikishiwa madai hayo na kutakiwa kuchukua hatua.


BMT kupitia kwa Kaimu Katibu Mtendaji, Neema Msitha, akiwa kwenye Michezo ya UMITASHUMTA mjini Mtwara, alitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kwamba, ni kweli wamekuwa wakipokea malalamiko na serikali ina taratibu zake za kufanya kazi.


Msitha alisema, si kweli kwamba Bayo hakuwasilisha kabisa vyeti vyake vya kielimu wakati akigombea, aliwasilisha isipokuwa uhalali wake ndio bado wanaufanyia kazi.


Kutokana na msukumo wa wadau hao kuzidi, Rais wa AT Silas Isangi, wiki iliyopita aliamua kuitisha kikao cha wadau jijini Arusha na kuzialika pande zote ili kulimaliza sakata hilo.     
Katika kikao hicho, Isangi alieleza azma yao ya kufanya mabadiliko ya katiba hususan kipengele cha elimu.


Isangi, aliponda uongozi wa AT uliokuwa madarakani kwamba haukuwa makini na kukubali kufanyika marekebisho ya katiba hiyo kwa maelekezo ya BMT.


"Unajua wenzetu hawakuwa makini wakaruhusu katiba hii ya BMT...Mimi nashangaa, CCM ni lichama likubwa na wakati wa uchaguzi niligombea ubunge kura hazikutosha, sifa ya kugombea ni kujua kusoma na kuandika, sisi tutafanya marekebisho kurekebisha haya," alisema Isangi.


Isangi, aliwataka wadau wawaache wafanye kazi hadi kipindi chao kimalizike, na endapo kuna jambo wamuone kwani yeye ni muwazi.


Hata hivyo katika kikao hicho, baadhi ya wadau walikisusia kuhudhuria wakidai katiba iheshimiwe.


Mmoja wa wadau hao, Wilhelm Gidabuday, alidai hakuhudhuria kwa kuwa hataki kuwa sehemu ya wanaosigina katiba.


Gidabuday ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa AT, amekuwa mstari wa mbele kudai Bayo hana sifa kwa mujibu wa katiba na kwamba kuna baadhi ya watu wanamkingia kifua.


Mdau huyo, alisema ikiwa katiba hiyo ilitumika kuwaengua bàadhi ya wagombea, inakuwaje kwa Bayo isifanye kazi.
Gidabuday, alithibisha kuwa ameandika barua kwa Waziri Bashungwa, akiomba sheria na kanunj ziheshimiwe bila kumbeba mtu.


Hata hivyo, wadau mbalimbali wameonyesha kushangazwa na kauli ya Isangi ya kunuia kufanya mabadiliko ya katiba kipindi cha sakata hili.

No comments:

Post a Comment

Pages