June 17, 2021

RC Makala afanya ziara ya Ukaguzi miradi ya DMDP Temeke, awataka wakandarasi kuikamilisha kwa wakati


 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, akiwa katika ziara ya kukagua Miradi ya Kimkakati (DMDP) iliyopo wilayani Temeke.




Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala amefanya ziara ya kukagua Miradi ya Kimkakati ( DMDP) iliyopo wilayani Temeke na kuwataka Wakandarasi waliokabidhiwa miradi hiyo kutekeleza makubaliano walioingia kwa kuikamilisha kwa wakati uliopangwa kwani watakaoshindwa hawatapewa miradi mingine.

Katika ziara hiyo RC Makala amekagua Mradi wa Barabara ya  Mwele iliyopo Kata ya Mbagala, Barabara ya Kliniki, pamoja Barabara ya Nzasa kupitia Buza hadi Kilungule katika Kata ya Kilungule yenye gharama ya Sh Bilioni 19.1.

RC Makala amesema miradi yote ya DMDP itafanyiwa tathmini na wakandarasi watakaobainika kushindwa kukidhi matakwa yaliyopo kwenye mikataba waliyoingia na Serikali hawatapewa miradi ya awamu nyingine.

Akiwa katika Kata ya Kilungule RC Makala alimuagiza mkandarasi aliyekabidhiwa barabara hiyo kufanya kazi katika muda uliopanga la sivyo akishindwa hatopewa miradi mingine ya kimakakati.

Amebainisha kuwa mkandarasi mwenye dhamana ya barabara hiyo atumie busara na ubinadamu kwa kuwapangishia wananchi waliopo karibu na ujenzi wa barabara kwao wengi wameathirika na vumbi na udongo ulioingia majumbani mwao. 

Ameongeza kuwa wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa wakandarasi kwa kufikia mwafaka kabla hawajapangiwa vyumba maeneo mengine na kwamba madhara yakiongezeka eneo itabidi walipwe fidia.

RC huyo amesema tayari Seriakali imetoa Sh bilioni 5 katika ujenzi wa   barabara ya Kliniki hivyo Kampuni ya JASCO iendelee na ujenzi huku kiasi cha fedha kilichobaki kikiendelea kushughulikiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe amesema maelekezo yote yaliyotolewa na RC Makala yatatekelezwa ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati.

Aidha, amesema Serikali imetoa Sh Bilioni 216.7  na kwamba hadi sasa Sh Bilioni 165.3 zimeshalipwa kwa wakandarasi huku akisisitiza miradi hiyo ikikamilika itasaidia kupunguza msongamano katika Barabara ya Kilwa.

Naye Diwani wa Kata ya Kilungule Said Fella ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za mradi wa barabara unaopita katika kata yake kwani utasadia kutoa ahueni ya msongamano wa magari kwa wananchi wanaokwenda Chamazi.


No comments:

Post a Comment

Pages