June 24, 2021

RIDHIWANI KIKWETE; "LEO NIMESEMA 'NDIYO' KWENYE KUPITISHA BAJETI YA SERIKALI BUNGENI"

-Atoa sababu 6 kwa Wananchi wake wa Chalinze


Na Andrew Chale

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapa neno la tumaini Wananchi wa lake la Chalinze na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa miongoni mwa Wabunge waliopitisha bajeti ya Serikali katika Bunge la Bajeti linaloendelea, Jijini Dodoma.

Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia mitandao ya Kijamii mbalimbali, Mhe. Ridhiwani Kikwete aliandika:

"Wana Chalinze na Watanzania wenzangu, leo nimesema 'NDIYO' kwenye kupitisha Bajeti ya Serikali Bungeni, Dodoma.
 
Nimefanya hivyo kutokana na sababu nyingi lakini kubwa ni kwamba ninaamini katika nia njema aliyonayo Rais wetu Mhe. Samiah Suluhu Hassan na wote wanaomshauri.

Pili, ni ukweli kuwa, Bajeti hii inalenga kutengeneza mazingira mazuri ya Biashara na ufanyaji wa kazi zitakazosaidia Watanzania kupata kipato chao.
 
Tatu, Bajeti imeangalia vijana katika nyanja mbalimbali kuanzia kujiajiri, kuwezeshwa, mawasiliano, michezo etc.

Nne, imeangalia makundi ya wakina mama na utatuzi wa changamoto zao na za Watoto kiafya, uwezeshaji, mazingira wezeshi elimu na haki zao za kumiliki vyanzo vya kiuchumi.

Wazee, kupitia miradi ya TASAF na Afya kwa wote wanakwenda angaliwa nao na maslahi makubwa yanaangaliwa.

Tano, miradi yetu ya maji inaaangaliwa. Kupitia bajeti fedha zinazopelekwa kwenye Mawakala wa Maji Vijiji -Ruwasa wameongezewa na mradi wetu kama ule wa Kibindu (Jimboni) umeanza kushughulikiwa na huku miradi mingine ikiongezewa pesa ili ikamilike mapema zaidi.

Sita, idara za kuwezesha wananchi wetu kama Kilimo, Ardhi, zimewezeshwa fedha  nyingi zaidi kuwezeshwa ununuzi wa teknolojia za kisasa kuwezesha upimaji, upangaji na miradi ya umwagiliaji.

Hizo kwa uchache na nyengine zikiwemo jinsi anavyoshughulikia mapambano na magonjwa kama Corona, maboresho na uwezeshaji vifaa katika Mahospitali yetu, anavyojenga miundo mbinu ikiwemo Daraja la kihistoria la Busisi, Bwawa la kuzalisha Umeme la Nyerere, mradi wa gesi -Lindi na kuimarika kwa Mahusiano na Majirani na Nchi marafiki kama China, Marekani, Uingereza, Afrika Kusini ni wazi nilishawishika kupiga kura ya 'NDIYO'." Aliandika Ridhiwani Kikwete na kuongeza kuwa;

"Nasimama nikiwaomba Wananchi wenzangu tuendelee kumuunga Mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan mwenye Maono na atakayetuvusha kuelekea ile nchi ambayo wazee wetu walitamani kuona tunaifikia. Mwenyezi Mungu amlinde Rais wetu, Ailinde Nchi Yetu, Atulinde Sote pia.

Usiku mwema kwetu sote."Alimalizia Ridhiwani Kikwete katika andiko lake hilo kwenda kwa Wananchi  wa Jimbo lake na Watanzania kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment

Pages