June 23, 2021

SERIKALI HAINA MPANGO NA KILIMO CHA BANGI

 


 

Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

SERIKALI imesema kuwa haina mpango wa kuruhusu kilimo cha bangi kwa sasa, huku ikiwataka Watanzania kulima mazao mengine ambayo yanamahitaji makubwa katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kamishna Generali wa Mamalaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) Gerald Kusaya, alibainisha hayo leo  jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na dawa za kulevya Duniani.

Kusaya, amesema kuwa siku hiyo ambayo huadhimishwa Juni 26, ya kila mwaka kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani Dodoma huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri mkuu Kassim Majaliwa.

Akizungumzia kilimo cha bangi ambacho baadhi ya wanasiasa hivi karibuni wamekuwa wakitoa maoni yao kiruhusiwe kulimwa alisema serikali bado haiko tayari kuruhuzu wananchi kulima kama mazao mengine.

“Mazao ya biashara nchini tunayo zaidi ya 95, ukichukua alizeti pekee yake tuu bado hatujalima vya kutosha ndiyo maana leo hii taifa linaagiza mafuta ya kula kutoka nje na kutumia bilioni 500 kila mwaka lakini pia bado yapo mahitaji ya zao la shairi lakini Misri wanahitaji pia mahindi ya njao”alisema Kusaya

Aidha, alisema kuwa kila mtu nayohaki ya kutoa maoni yake lakini jambo la msingi ni kwa Watanzania kuona fursa zilizopo katika mazao mengine na siyo kuunga mkono kilimo cha bangi.

“Hii bangi hata ikiruhusiwa leo sio kila mtu atalima labda taasisi fulani ndiyo itahusika lakini pia hata hayo mataifa mengine yanayolima bangi siyo kama hii ambayo inaharibu akili za watu ipo nyingine kwani zipo aina nyingi za bangi”alisisitiza Kusaya

Akizungumzia kuhusu hali ya udhibiti wa dawa za kulenya nchini, Kusaya alisema kuwa nchi ipo katika kiwango kizuri cha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

“Sisi kama taifa vipo vyombo ambavyo vipo juu yetu vinavyotuangalia na kututathimini tumefanya kwa kiasi gani kudhibiti matumizi pamoja na usambazwaji wa dawa hizi, kwamujibu wa ripoti iliyotolewa 2019/20 inaonyesjaha kuwa sisi Tanzania tumedhibiti dawa za kulevya kwa zaidi ya asilimia 90.

“Hivyo utaona kuwa tupo katika hatua nzuri lakini pia hivi sasa toka nimeingia madarakani tumeweka uangalizi wa juu sana ndiyo maana tulifanikiwa kukamata kiasi kikubwa sana cha dawa toka tupate uhuru ambacho ni kilo 856.39 za dawa za kulevya”alisema Kusaya

Pia, alisema kuwa kama kila Mtanzania atachukia vitendo vya biashara ya dawa za kulevya taifa litafanikiwa kupiga hatuka katika mapambano hayo na kuokoa nguvu kazi inayoteketea.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka aliwataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanaja vya Nyerere squre kuanazaia leo.

“Wananchi waje kwa wingi kwakuwa kutakuwepo na utoaji wa elimu mbalimbali juu ya athari za utumiajia wa dawa za kulevya kuanzia juni 24 na maonyesho ya wajasiriamali mbalimbali kabla ya kilele cha siku hiyo kitaifa Juni 26,”alisema Mtaka

No comments:

Post a Comment

Pages