June 04, 2021

Serikali kuwawekea mazingira wezeshi Sekta Binafsi



Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Emmanuel Tutuba akizungumza na wahariri wa vyombo vya Habari  wakati  akifungua semina ya siku 2 kwa wahariri hao kuhusu masuala ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ambapo ametoa wito kwa wahariri hao kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya ubia, Jijini Arusha.

 

NA BETTY KANGONGA


SERIKALI imeahidi kuwawekea mazingira wezeshi sekta binafsi ili waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi kwa utaratibu wa ubia Kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).

Hayo yalibanishwa jana jijini Arusha na Katibu Mkuu Wizara Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba wakati akifungua Mafunzo kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuhusu utekelezaji wa programu ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

Tutuba alisema, Serikali iliandaa programu hiyo ya PPP nchini ili kuwezesha sekta binafsi kushirikiana na serikali kwa utaratibu wa ubia katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za uchukuzi, Ujenzi, Elimu, Afya , Mawasiliano, Maji, Michezo, Viwanda na Biashara.

Alisema mwelekeo  huu wa PPP unashabihiana na mipango iliyowekwa na nchi nyingi za Afrika na nje ya Afrika kutumia sekta binafsi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Dhana PPP sio ngeni kwa Tanzania , kabla ya kutungwa kwa sera hii mwaka 2009 Serikali ilihusisha sekta binafsi kutekeleza baadhi ya miradi, mfano miradi ya IPTL , City Water, na RITES- India," 

"Hata hivyo miradi haikufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa mazingira wezeshi yenye kuelekeza taratibu za kufuata katika kufanya maandalizi kabla ya kuingia mikataba ya PPP kwa lengo la kuleta tija na manufaa kwa Taifa," alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema hadi sasa jumla ya miradi  41 imeandaliwa na kufanyiwa uchambuzi ambapo Kati ya miradi hiyo 40 imeandaliwa na mamlaka za Serikali kutoka sekta mbalimbali na mradi mmoja umeandaliwa na mwekezaji kutoka sekta binafsi .

Alisema mfumo huo wa PPP nchini una umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maendeleo,  ujenzi wa miundombinu na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa jitihada hizi zitachangia kujenga uchumi shindani na wa viwanda kwa maendeleo ya watu ifikapo mwaka 2025/2026, faida zingine ni kupata utaalamu wa teknolojia kutoka sekta binafsi na kupata ufunifu, kuongeza ubora wa huduma,kuongeza wigo wa bajeti katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

"Kwamfano upande wa Nishati, wapo watu wanatengeneza shamba la umeme wa jua, mtu anazalisha umeme wa jua na anaiuzia serikali, ujenzi na barabara za lami, madaraja na hospitali,  wananchi wanafaidika, muwekezaji anafaidika na Serikali pia inapata faida," alisema.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itahakikisha miradi iliyopangwa kutekelezwa katika programu hiyo ya PPP zinafanyiwa uchambuzi wa timu za wataalamu zinazoundwa kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake Kamishna PPP Dk. John Mboya alisema, ili kufikia azma ya kutekeleza programu ya PPP na kwa kasi inayotakiwa wanatoa elimu kwa umma kuhusu dhana ya programu hiyo ili wadau wote waweze kushiriki kikamilifu ili waweze kitekeleza sera na sheria ya PPP.

"Elimu hii imekuwa ikitolewa ambapo kabla ya mwaka huu wa fedha jumla ya wadau 829 walipatiwa elimu, waliohusika ni pamoja na watumishi wa wizara ya fedha, idara zinazojitegemea, Taasisi za umma, Wabunge , Makatibu wakuu, na Wakurugenzi wa halmashauri," alisema .

Alisema kuhamasisha utoaji wa elimu kwa mwaka huu wa fedha wizara inatoa elimu kwa Wahariri wa vyombo vya Habari 38 ili wapate taarifa sahihi kuhusu dhana ya PPP na waweze kuelimisha jamii na wadau mwengine.


No comments:

Post a Comment

Pages