Na WAMJW - Dodoma
Kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika, Serikali inatarajia kuzindua Makao ya Taifa ya Malezi na Makuzi ya Watoto yaliyojengwa katika Kata ya Kikombo, jijini Dodoma.
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Dkt Dorothy Gwajima amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Isdor Mpango atazindua makao hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu.
Dkt. Gwajima amesema lengo la kujengwa kwa makao hayo ni kutatua changamoto za makao ya Taifa ya awali yaliyokuwa Kurasini Dar es Salaam za ufinyu wa maeneo ya shughuli mbalimbali ikiwemo michezo, bustani, ujasiriamali na ufugaji kutofanyika sawasawa hivyo kufanya hali ya lishe na uchumi kuwa duni.
" Ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Kimkakati wa kuwatambua, kutengamanisha na kuwaunganisha na familia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, pia ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais kuwa watoto wanaotunzwa kwenye makao waandaliwe mapema kadri inavyowezekana kuwaunganisha na familia ili kuwawekea msingi wa malezi" alisema Dkt. Gwajima.
Ameongeza pia watoto wanatakiwa kukaa kwenye makao kwa muda tu na wakiisha kuimarika warejeshwe kwenye makazi ya kawaida iwe ya kambo au kuasili ili waishi kawaida katika familia.
Dkt. Gwajima amesema, uzinduzi huo utaambatana na uzinduzi wa vituo vya Jamii vya malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya watoto pamoja na Baraza la Taifa la Watoto hapo tarehe 14 mwezi huu.
Aidha, Dkt. Gwajima ametoa rai kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatimiza jukumu la malezi ya watoto wao na kuwa, hatua ya kulelewa katika makao iwe ni ya mwisho baada ya hatua zote kushindikana.
Mradi wa Ujenzi wa Makao ya Watoto Kikombo, umetekelezwa kwa Ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto na Shirika la ABBOT Fund Tanzania na Makao hayo yana uwezo wa kuhudumia watoto 250 kwa wakati mmoja na hadi sasa watoto wanaohudumiwa katika Makao hayo ni 28.
No comments:
Post a Comment