June 22, 2021

SINGIDA YATENGA ZAIDI YA EKARI 666, 444 KWA AJILI YA KILIMO CHA ALIZETI


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge, akizungumza na  wadau mbalimbali wakati akifungua kikao cha wadau wa kilimo cha Alizeti kilichofanyika mkoani hapa leo.

Wadau wa kilimo wakiwa kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchakata alizeti wakiwa kwenye kikao hicho. 
Maafisa wa Jeshi la Magereza wakiwa kwenye kikao hicho.
 
  
Na Dotto Mwaibale, Singida


MKOA wa Singida umetenga jumla ya ekari 666,444.3 kwa ajili ya eneo linalotarajiwa kulimwa zao la alizeti.

Hayo yamebainishwa na Mkuu Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge wakati akifungua kikao cha wadau wa kilimo cha zao hilo kilichofanyika jana mkoani hapa.

Dkt.Mahenge alisema lengo la kikao hicho nikuhamasisha kilimo hicho mkoani hapa ili kufikia jumla ya tani za mafuta ya alizeti zinazohitajika nchini ambazo ni takribani tani 670,000 ili kukidhi mahitaji ya mafuta nchini.

" Ili kufikia malengo hayo mkoa umependekeza Serikali kutoa ruzuku ya mbegu bora zenye ujazo wa tani 1333 kwa wakulima na kuboresha mfumo wa masoko wa zao la alizeti ili kuwahakikishia wakulima wanapata bei nzuri," alisema Mahenge.

Alitaja mapendekezo mengine kuwa ni Serikali kuanzisha bodi ya mazao ya mafuta, kuanzisha mashamba darasa ya kuzalisha mbegu bora, taasisi za fedha ziwezeshe wakulima wakubwa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa mikopo ya masharti nafuu na itenge fedha kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji ya uzalishaji wa mbegu za alizeti.

Alisema hatua hiyo itapunguza upatikanaji wa mbegu kwa gharama kubwa na kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti.

Akichangia kwenye kikao hicho Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliishauri Serikali kupitisha zoezi la upimaji wa ardhi za vijiji kwa lengo la kufanikisha wakulima kupata mikopo kupitia mashamba yao.

Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Grace Masambaji alisema vyama vya ushirika ambavyo vitapata ruzuku ya Serikali kwa ajili ya kilimo cha alizeti ni vile vilivyokidhi vigezo vya usajili na si vinginevyo.

Mkulima Hamisi Samade kutoka Itigi akichangia katika kikao hicho alisema utoaji wa mikopo kupitia mabenki umekuwa ukichelewesha sana hivyo kuwakwamisha wakulima ambapo pia aliomba mikataba ya mikopo wanayopatiwa na mabenki, vyama vya ushirika (AMCOS) na wadau wengine iandikwe kwa lugha ya kiswahili ili waweze kuielewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Benki ya Maendeleo (TIB) Patrick Mongella alisema ni vizuri wakulima wajiunge katika vikundi ili taasisi za kifedha ziweze kuwakopesha kirahisi kuliko kutoa mikopo hiyo kwa mkulima mmoja mmoja ambapo panakuwa na changamoto ya kuirejesha.

Baadhi ya wadau walioshiri kikao hicho ni halmashauri zote, wamiliki wa viwanda vya kuchakata alizeti vya Biosustain, Sunshine, Kongano Mtinko, Mount Meru, Magereza-Ushora na Taasisi za kifedha Benki ya NMB, TPB, CRDB,TIB, TADDB, NBC na PASS. 

No comments:

Post a Comment

Pages