June 10, 2021

Wadau wa Elimu wajadili Mchango wa Mwalimu Nyerere Kongamano la Miaka 50 la Elimu ya Watu Wazima

Ndubikile, Dar es Salaam

 

Wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejadili mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika harakati zake za kuendeleza elimu ya watu wazima nchini na kimataifa wakihimiza kuendelezwa kwa juhudi hizo ili kupunguza kundi la watu wasiojua kusoma na kuandika.

Hayo yamesemwa na wadau hao jijini Dar es salaam katika Siku ya pili ya Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Shule Kuu ya Elimu ya chuo hicho.

Akiwasilisha mada katika kongamano hilo Aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya misaada ya kijamii ikiwemo elimu ya watu wazima (DVV} Prof Heribert Hinzen amesema mchango wa hayati Nyerere katika kuiendeleza na kuipigania elimu hiyo ni mkubwa kwani mwaka 1970 alitangaza kuwa mwaka rasmi wa kuanza kutolewa ili kupunguza maadui watatu wa wa Nchi ikiwemo Ujinga,umasikini na Maradhi.

Prof Hinzen amebainisha mwaka 1974 mwalimu Nyerere alisisitiza katika maeneo yote ya nchi elimu hiyo itolewe bila kujali ubaguzi wowote ambapo kwa kiasi kikubwa ilisaidia kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma,kuhesabu na kuandika pamoja na stadi za maisha.

Amefafanua kuwa utoaji wa elimu hiyo unatakiwa kuendelezwa na serikali pamoja na wadau wengine binafsi wa elimu kuhakikisha wanafanya juhudi zaidi kuwafikia watu wengi walio maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Bayero kilichopo Jimbo la Kano nchini Nigeria,Hafsat Umar aliyewasilisha mada ya utolewaji elimu ya ujasiriamali bila kujali ubaguzi  ilivyochangia makundi ya vijana na Wanawake walivyojiajiri katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuku hivyo alisisitiza kuwa Tanzania inatakiwa kutoa elimu ya watu wazima kwa kuangalia fursa za kimazingira.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Elimu Mkwawa [MUCE] Daktari Adelle Raymond amesema jamii ya wafugaji nchini inatakiwa kutengenezewa mitaala ya elimu ya watu wazima ambayo itaweza kulifikia kundi hilo kwani limekuwa na tamaduni za kuhamahama kutafuta malisho ya mifugo yao hivyo watoto na watu wazima hukosa fursa ya kujikomboa kielimu.

Mwanafunzi wa Stashahada ya Uzamili wa shule hiyo Vale Adam aliyewasilisha mada ya mtazamo wa waajiri kuhusu watu wenye mahitaji maalum amesema waajiri wanatakiwa kuondoa fikra potofu kwa  kulipa nafasi Kundi hilo bila ubaguzi kwani lina uwezo wa kutekeleza majukumu yake sehemu za kazi.

Katika siku ya pili ya mwendelezo wa Kongamano hilo lenye Kauli mbiu isemayo Elimu ya Watu Wazima kwa Maendeleo  Endelevu Tanzania Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo hicho Profesa Elusesa Bhalalusesa alikuwa mwenyekiti katika mada zilizowasilishwa na wadau mbalimbali.

Katika ufunguzi wa Kongamano hilo Mgeni Rasmi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa maagizo tisa kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu ya Watu nchini, na UDSM ikiwemo kufanya tafiti za mahitaji ya elimu hiyo na kuja na njia za kukabiliana na matatizo yanayoikabili  pamoja kutoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kufufua madarasa ya elimu hiyo (MEMKWA).

No comments:

Post a Comment

Pages