Na Dotto Mwaibale, Singida
ZAIDI ya Wanawake 2300 wilayani Ikungi mkoani Singida wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kilimo cha alizeti na mbogamboga kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Japani (KOICA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na usawa wa kijinsia na wanawake (UN Women)
Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya siku moja ya maofisa wa mashirika hayo ya kukagua mradi uliopo katika Kata ya Dung'unyi, Sepuka na Irisya wilayani hapa ili kuona utekelezaji wake na matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Koica ambapo wameridhishwa na utekelwezaji wa awamu ya kwanza wa mradi huo.
Mradi huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka jana mkoani hapa unatekelezwa na mashirika hayo, Serikali ya Tanzania, Farm Africa na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA katika mikoa ya Singida na Shinyanga.
Akizungumza katika ziara hiyo Mtaalamu wa Kitengo cha Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kutoka UN Women, Lillian Madanga alisema wanafanya kazi hiyo kisera kwa kushirikiana na Serikali, Sekta binafsi na Halmashauri ambazo wana miradi hiyo yenye lengo la kuwainua wanawake kiuchumi kupitia kilimo cha mbogamboga matunda na alizeti.
Alisema katika kilimo cha mbogamboga na matunda wanafanya kazi na TAHA ambao wanauzoefu mkubwa na kilimo hicho hapa nchini kwa ufadhili wa Koica ambao wametoa fedha na kuwa kwa siku za mbeleni wananchi wa Ikungi watabadilika kimaendeleo kupitia kilimo hicho.
"Lengo letu kubwa la kuanzisha kilimo hiki na kuwapa teknolojia na kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi," alisema Madanga.
Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumza katika ziara hiyo aliishuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha hizo katika wilaya hiyo na kuwa watafanya kila liwezekanalo na kuona kilimo hicho kinanakuwa endelevu na kinawapeleka mbele.
Aidha Kijazi alisema kuwa mradi huo utagharimu zaidi ya Sh.Bilioni 5.2 na kuwa umegawanyika katika aina kuu tatu, kilimo cha alizeti ambacho kinaongozwa na Farm Africa, Kilimo cha mbogamboga kinachoongozwa na TAHA na Mradi wa kuwawezesha wanawake kijinsia.
Alisema kwa mwaka huu wa mradi takribani dola 900,000 zimeruhusiwa na Koica na zinaendelea kufanya kazi katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Alisema mradi huo utakuwa kichocheo cha maendeleo katika halmashauri hiyo na kioo ambapo watatarajia kupata wawekezaji wengi baada ya kuona ardhi ya wilaya hiyo kuwa na rutuba ambayo kila aina ya mazao yanastawi.
Alisema jambo kubwa wanalolifanya hivi sasa ni upimaji wa ardhi katika vijiji vinne ambavyo wanavipima kupitia fedha za mradi huo ambavyo ni Kipumbwiko, Irisya, Munyu na Mnang'ana.
"Katika vijiji hivyo tunatenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya kilimo, makazi, misitu na ufugaji jambo litakalotusaidia kujua iwapo akitokea mwekezaji wa eneo husika kati ya haya yaliyotajwa tujue kwa kumpeleka," alisema Kijazi.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha inafanya mradi huo Msalala mkoani Shinyanga na Ikungi mkoani Singida na imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi ambapo katika wilaya hiyo wameweza kuanzisha mashamba darasa .
Alisema katika wilaya hiyo wameweza kuwapa wakulima teknolojia za kisasa za kilimo cha mbogamboga, matunda, maembe,vitunguu, pilipili kichaa, matumzi ya mbegu bora na kuwa wamepata soko nje ya nchi na mnunuzi wa mazao hayo zikiwemo pilipili atakazo zinunua kwa Sh.6000 kwa kilo.
Aliwataja wadau wanao wawezesha katika mnyororo huo wa thamani kuwa ni wasambazaji wa pembejeo, wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na makampuni yanayofanya usafirishaji nje ya nchi na wanawawezesha kwa vitendo.
" Katika uwezeshaji wetu kazi kubwa tunazozifanya ni kuwaunganisha wakulima na masoko, kuwawezesha wakulima katika suala zima la kilimo na kuwaonesha teknolojia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kulingana na uwezo na mazingira waliopo." alisema Mkindi.
Alitaja kazi ya nyingine kuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kuwa wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kwa maana ya kushawishi na kutetea sera zile ambazo zinamuumiza mzalishaji, mfanyabiasha na mdau yeyote katika mnyororo wa thamani.
Aidha Mkindi alitaja kazi nyingine kuwa ni kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na vyombo vya fedha baada ya kuwafundisha elimu ya fedha.
No comments:
Post a Comment