June 17, 2021

WAZIRI WA NISHATI AZINDUA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME AWAMU YA PILI KATIKA MAENEO YA PEMBEZONI MWA JIJI LA DODOMA

 


Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzinduzia Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika Maeneo ya Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, katika kata ya Chihanga jijini Dodoma tarehe 16 Juni, 2021. Kushoto kwa Waziri kalemani ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, anayefuatia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mha. Amos William Maganga na kulia kwa Waziri Kalemani ni Mbunge wa jimbo la Dodoma mjini, Mhe. Anthony Mavunde.

 

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akimtambulisha Mkandarasi wa Mradi (Ceylex Engineering (PVT) LTD) na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa uongozi wa Mkoa wa Dodoma na kwa wananchi wa kata ya Chihanga, kijiji cha Chihanga, Dodoma wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika Maeneo ya Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, tarehe 16 Juni, 2021.


Wananchi wa kata ya Chihanga, kijiji cha Chihanga, Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika Maeneo ya Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, tarehe 16 Juni, 2021.


Na Dorina Makaya - Dodoma


Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, tarehe 16 Juni, 2021, alifanya uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika Maeneo ya Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, katika kata ya Chihanga jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi wa kata ya Chihanga, kijiji cha Chihanga, Dodoma, Dkt. Kalemani aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme kuboresha maisha yao kwa kuutumia kwenye miradi ya uzalishaji mali, ufugaji, pamoja na huduma mbalimbali za kijamii ili uwekezaji wa Serikali kwenye ujenzi wa miundombinu ambayo inatumia gharama kubwa uwe na tija.

Dkt. Kalemani, aliwaeleza wananchi wa kata ya Chihanga kuwa, shughuli mbalimbali za uzalishaji ambazo wanaweza kuzifanya ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano na kuboresha thamani za bidhaa zao za kilimo na viwanda.

Waziri Kalemani alisema, Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika Maeneo ya Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, utatekelezwa katika kata 16 katika mkoa wa Dodoma kwa muda wa miezi 12 ambapo kiasi cha shilingi za kitanzania takribani bilioni 17.3 zitatumika kuwafikishia umeme wateja wa awali 4,604 katika Mkoa wa Dodoma na kuwa fedha hiyo imetolewa na Serikali.

Alimtaka Mkandarasi wa Mradi huo, kukamilisha uunganishaji wa umeme katika kata ya Chihanga ndani ya mwezi mmoja na nusu na kuwa atarudi kuwasha umeme katika kata hiyo baada ya kipindi hicho.

Waziri Kalemani aliwahimiza wananchi watakaounganishiwa umeme kupitia Mradi huo, kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao (wiring) mapema ili mkandarasi atakapofika katika maeneo yao wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.

Alisisitiza kuwa, gharama ya kuunganishiwa umeme ni shilingi 27,000 tu na kueleza kuwa mradi huo utatoa fursa kwa vijana wa kata zitakazohusika wakati wa utekelezaji wa Mradi zitakazohitaji nguvu kazi kwani watatumika vijana wa maeneo husika.

Aidha Waziri Kalemani aliwaambiwa wananchi wa Chihanga na wale wote watakaohusika na kuunganishiwa umeme kupitia Mradi huo kuwa, kwa wale ambao utandazaji wa nyaya utakuwa haujakamilika ambao nyumba zao si kubwa (nyumba isiyozidi vyumba vitatu) wanahimizwa kuomba kufungiwa kifaa cha UMETA (Umeme Tayari) ili kuhakikisha wanapata huduma muhimu ya umeme.

Waziri Kalemani alisema, kifaa hicho cha UMETA hakihitaji kutandaza nyaya katika nyumba yote na kinatolewa bure kwa wateja 250 wa awali na kwa wale watakaoomba kifaa hicho baada ya vifaa 250 kutolewa kwa wateja wa awali kuisha, vifaa hivi vinapatikana TANESCO kwa shilingi 36,000 tu.

Aidha Dkt. Kalemani alimtaka Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Dodoma kufungua ofisi ndogo ya TANESCO ili kuwaondolea adha wananchi wa Chihanga kwenda umbali mrefu kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme na huduma mbalimbali za TANESCO.

Kuzinduliwa rasmi kwa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika Maeneo ya Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, katika kata ya Chihanga jijini Dodoma, kulishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiwemo Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Josephat Maganga na Mbunge wa jimbo la Dodoma mjini, Mhe, Anthony Mavunde.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mha. Amos William Maganga, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati vijijini, Wakili Julius Bundala Kalolo na wataalam kutoka TANESCO na REA.


No comments:

Post a Comment

Pages