July 06, 2021

COSTECH yatakiwa kubiasharisha bunifu

 

 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza katika majadiliano wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki.
 
Mbunifu Lulu Ameir kutoka Kampuni ya Bela Vendor Tanzania.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akikata utepe wakati wa uzinduzi wa ripoti ya BUNI&DTBI.
 

 

Na Selemani Msuya

 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameitaka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kushirikiana na wabunifu mbalimbali ili kuhakikisha bunifu zao zinabiasharishwa ili zichochee ukuaji uchumi, maendeleo na huduma za jamii

Prof. Ndalichako ametoa rai hiyo kwa COSTECH wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo amesema kumekuwepo na kasi kubwa ya vijana kubuni mambo mbalimbali lakini asilimia kubwa ubunifu wao unaishia njia kwa sababu hakuna mkakati wa kubiasharisha bunifu husika ili ziweze kuwa endelevu.

“Lengo la bunifu ni lazima ziwe na matokeo chanya hivyo naomba sana COSTECH kuhakikisha Atamizi hizi ambazo zipo na zinazokuja mnazibiasharisha ili ziweze kugusa maisha ya wananchi,” amesema.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikitumia COSTECH kama kituo kikuu cha kupokea bunifu ila kwa sasa wameanzisha vituo vingine 17 ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya, Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na vingine lengo ni kuona wigo wa kutengeneza ajira nyingi kwa vijana kupitia bunifu mbalimbali.

Aidha, amesema kupitia ubunifu jumla ya kampuni 94 zimeanzishwa na kutoa ajira zaidi ya 600 kwa vijana wa Kitanzania na huduma kuwa bora.

Prof. Ndalichako ametolea mfano bunifu za Hakika Fertilizer, Magila Tech, Smart Lab na Bela Vendor ambazo zimebuniwa na vijana Wakitanzania na kuweza kutatua baadhi ya changamoto katika jamii, kutoa ajira na kuchangia mapato kwa taifa.

Amesema kauli mbiu ya Siku ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni ‘Mchango wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika kukuza Viwanda, Kuongeza Ajira na Kuendeleza Biashara ambapo wabunifu wameonesha kwa vitendo katika eneo hilo hivyo ni vyema COSTECH kuongeza nguvu zaidi kwa kuhakikisha bunifu hizo zinabiasharishwa.

Waziri amesema kupitia shuhuda ambazo zimetolewa na wabunifu vijana ameshawishika nay eye kufikiria kufanya ubinifu kwa kuwa ni fursa sahihi ya kuajiajiri.

“Huu ubunifu ambao umefanywa na vijana unaendana na tarajio la Rais Samia Suluhu Hassan kutaka kujenga ujuzi kwa vijana na katika eneo hilo vijana wameonesha uwezo hata mimi nashawishika kufikiria jambo ili nikistaafu niweze kujiajiri,” alisema.

Prof. Ndalichako amesema kupitia bunifu hizi amegundua kuwa ujasiri ni mtaji mkubwa zaidi kuliko fedha hivyo ni wakati wa kila kijana na mbunifu kuwa na uthubutu kwa kuwa uwezo upo kwa Watanzania wengi.

Aidha, alitoa wito kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi kuwaamini vijana ambao wamekuwa na uthubutu kwa kuwa hiyo ni njia ya kuwafungulia milango ya kutimiza ndoto zao.

“Vijana wangu mmeniheshimisha sana niwaahidi kuwa nitawaunga mkono kwa nguvu zote ili tuweze kuchochea ukuaji wa uchumi, maendeleo na huduma za jamii,” amesema.

Amesema Serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 45 kwa kipindi cha miaka mitano ili kuchochea eneo la ubunifu ambalo ni muhimu kwa ulimwengu wa sasa.

Ndalichako amewataka vijana wabunifu kutumia Kurugenzi ya Sayansi, Tenkolojia na Ubunifu na COSTECH kutatua changamoto ambazo zinapatikana kwenye michakato za bunifu zao.

“Mei 27 Wizara ya Fedha ilisaini msaada wa Dola Milioni 425 sawa na Shilingi Bilioni 970 kutoka Benki ya Dunia za kuendeleza elimu ya juu ambapo kati fedha hizo tumetenga dola milioni 19 sawa na shilingi bilioni 45 za kuendeleza eneo la ubunifu kwa miaka mitano,” amesema.

Akizungumza baada ya hotuba ya Waziri Ndalichako, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu amesema uwezeshaji vijana katika bunifu kumeweza kuitafsiri taasisi hiyo kwa kundi kubwa la vijana ambao walibakia mitani bila kuendeleza bunifu zao.

Dk.Nungu amesema vijana ambao wamewezeshwa na COSTECH wamekuwa wachangiaji wa mapato kwa Serikali hivyo wao wataendelea kuwawezesha vijana ambao wanakuwa na bunifu ambazo zinaweza kutoa matokeo chanya.

“Sisi tumejipanga kuwafikia vijana wabunifu kupitia Mashindano ya Kimataifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na kuwaendeleza ili waweze klutengeneza ajira, viwanda, kulipa kodi na huduma za jamii kwa maendeleo ya nchi,” amesema.

Wabunifu Ahad Katera (Hakika Fertilizer), Godfrey Magila (Magila Tech), Edwin Bruno (Smart Lab) na Lulu Ameir (Bela Vendor), wamesema COSTECH ni taasisi ambayo imewafungulia fursa za maisha yao na jamii.

Wamesema kwa sasa wameweza kuaminika, kuheshimiwa, kuajiri ndani na nje ya nchi ambapo COSTECH ndiyo imechochea mafanikio hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages