Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa wazawa na Uhusishwaji wa Wadau PURA, Charles Nyangi (kulia) pamoja na Mjiolojia Magambo Samwel (mwenye suti ya bluu) wakitoa uelewa wa masuala ya mkondo wa juu wa petroli kwa washiriki wa Maonesho ya Sabasaba waliotembea banda la PURA, Julai 7, 2021.
Na Selemani Msuya
WATANZANIA wametakiwa kujianda kushiriki katika miradi ya kuchimba visima vya mafuta na gesi kwenye mkondo wa juu ili wawe sehemu ya kuchangia ukuaji wa uchumi.
Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Ushiriki wa Wawazawa na Wahusishaji wa Wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi wakati akizungumza na Raia Mwema jana jijini Dar es Salaam.
PURA wanashiriki Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ' Uchumu kwa Ajira na Biashara Endelevu' yanayofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere Temeke jijini Dar es Salaam.
Nyangi alisema PURA inasisitiza Watanzania kujiandaa kushiriki kwenye miradi ya uchimbaji mafuta na gesi ili wawe sehemu ya kuongeza mnyororo wa thamani katika eneo hilo ambalo awali lilijukana kuwa ni fursa za watu wenye uwezo mkubwa.
Alisema fursa za uchumbaji mafuta na gesi katika mkondo wa juu ni nyingi hivyo wanapaswa kubadilika na kuamini kuwa wana uwezo wa kushiriki.
“Ni kweli awali Watanzania walikuwa wanafikiria kuwa miradi hiyo ni ya watu wenye uwezo lakini ukweli ni kwamba hakuna kisichowezekana iwapo wataamua kushiriki kwani fursa hii haingalii sura au utajiri wa mtu bali ni uwezo wa kutoa huduma.
Katika nchi zilizoendelea kwenye eneo hilo wazawa ndio washiriki wakubwa jambo ambalo linawezesha faida kubwa ya kinachopatikana kubakia nchi,” alisema.
Mkuu huyo wa kitengo alisema PURA inaendelea kutoa elimu kwa Watanzania wa kada zote kwa kuwa miradi kama hiyo inashirikisha kila mtu.
Nyangi alisema uwekezaji kwenye uchimbaji unahitaji wadau wengi kama wauzaji wa vyakula, vifaa vya uchumbaji, uasafirishaji hivyo ni jukumu la Watanzania wenye sifa kujitokeza fursa hiyo inapotekea.
Alisema katika mradi mmoja ambao ulitekelezwa hapa nchini Watanzania 52 walishiriki jambo ambalo linawapa matumaini ya kwamba wanachokisimamia kimeanza kueleweka kwa jamii.
Mkuu huyo wa kitengo alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho kuandaa kanzidata ambayo itaonesha watoa huduma, wafanyabiashara na wadau wote katika sekta.
Alisema kupitia kanzidata hiyo wataweza kumuelekeza mwekezaji anayetaka kuingia mkataba wa kuchimba mafuta na gesi kujua ni mzawa yupi ambaye ana sifa stahiki ili washirikiane.
Nyangi alisema eneo la mafuta na gesi ni muhimu katika maendeleo ya nchi hivyo anasisitiza wadau wengi kujitokeza kuwekeza katika kuchimba mafuta na gesi kwenye mkono wa juu wa petroli.

No comments:
Post a Comment