Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akipata maelezo kutoka kwa Mkufunzi wa Uhandisi Matengenezo ya Ndege kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Castory Njato, kuhusu bawa la ndege linavyofanyakazi baada ya kupokea vifaa vya kufundishia wanafunzi wa uhandisi wa matengenezo ya ndege kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akikata utepe ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya vifaa vya kufundishia.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof. Zacharia Mganilwa, akifafanua jambo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, kuhusu kifaa kinachotumika kufundishia wanafunzi mfumo wa bawa na tairi la ndege.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akipata maelezo kuhusu injini ya ndege inavyofanya kazi pamoja na kupima mafuta, joto na hewa inayoingia kwenye injini kutoka kwa Mkufunzi wa Uhandisi Matengenezo ya Ndege, Castory Njato.
Dar es Salaam, Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetoa vifaa vya kufundishia kozi ya uhandisi wa matengenezo ya ndege vyenye thamani ya Sh. Mil. 445.4 kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema nchi inahitaji kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta ya usafirishaji hasa wa anga.
Amesema TEA imetoa ufadhili wa fedha hizo kwa ajili ya kuwezesha ununuaji wa vifaa hivyo vitakavyotumika kuwafundishia wanafunzi wanaosomea uhandisi wa matengenezo ya ndege.
"Kwenye ndege sasa hivi tunafanya vizuri hivyo tunahitaji wataalamu wa kutosha watakaokuwa wanatengeneza ndege pindi zinapoaribika hivyo vifaa hivi vya mafunzo ni vya kisasa na vyenye ubora wa hali ya juu nina amini vitakidhi mahitaji ya mafunzo ya taaluma ya uhandisi wa matengenezo ya ndege," amesema.
Aidha vifaa hivyo vitakiongezea chuo uwezo wa kutoa elimu bora zaidi hususani kwenye sekta ya usafirishaji upande wa anga na kuongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha vyuo vya kimkakati kama NIT vinatoa mafunzo yanayo akisi maendeleo ya wananchi yanayolenga kutatua changamoto zinazowakabili.
Aidha alisema vifaa hivyo vimegharimu fedha nyingi za walipa kodi hivyo vinatakiwa kutunzwa vizuri na kutumika kwa uangalifu ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha walengwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bahati Gauzye, amesema ununuzi wa vifaa hivyo umefanikiwa kupitia ruzuku iliyotolewa na Wizara ya Elimu kupitia mfuko wa elimu baada ya NIT kuwasilisha maombi ya ruzuku kwa ajili ya vifaa vya kufundishia.
"Ruzuku iliyotolewa kwa NIT ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la msingi la mfuko wa elimu ya taifa unaosimamiwa na TEA, kupitia mfuko huo ufadhili ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu na ununuzi wa vifaa hutolewa katika ngazi zote za elimu kwa Tanzania bara na elimu ya juu kwa Tanzania Zanzibar," amesema.
Ufadhili huo uliyotolewa na TEA kupitia wizara hiyo utawasaidia vijana wengi wenye ndoto za kuwa wanataaluma katika sekta ya usafiri wa anga kupata masomo hapa hapa nchini tena kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha NIT, Prof. Zacharia Mganilwa amesema vifaa vilivyopokelewa ni vinne ambavyo kimoja ni kwaajili ya kufundishia wanafunzi mfumo wa bawa na tairi la ndege.
Alisema kifaa kingine ni kwaajili ya kumfundisha mwanafunzi namna injini ya ndege inavyofanya kazi pamoja na kupima mafuta, joto na hewa inayoingia kwenye hiyo injini.
"Kifaa hicho pia mwalimu anaweza kukitega ili hewa isiweze kuingia sasa hapo mwanafunzi anatakiwa kujua tatizo hilo na kuweza kulirekebisha ili hewa iweze kuingia na mfumo ukae sawa," amesema.
Prof. Mganilwa alisema vifaa hivyo walivyovipokea vitawasaidia wanafunzi kuweza kujifunza masomo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege kwa vitendo.
No comments:
Post a Comment