September 02, 2021

Dk. Akwilapo aongoza wadau kutathimini ya maendeleo ya elimu


Mwenyekiti wa Bodi kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania TEN/MET, Lydia Wilbard ambaye ni miongoni mwa wadau walioshiriki katika mkutano huo.

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akizungumza katika  mkutano huo Jijini Dar es salaam leo
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mtaa TAMISEMI, Gerald Mweli  akizungumza na wadau wa Elimu kutoka Taasisi mbalimbali binafsi na Serikali
Baadhi ya wadau walioshiriki katika mkutano huo ambao unafanyika kwa siku mbili

 

Na Mwandishi Wetu

 

WADAU wa Elimu kutoka Taasisi za Serikali na binafsi leo wamekutana kujadili na kutoa maoni kuhusu tathimini ya maendeleo katika sekta ya elimu.

Mkutano huo uliondaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umetoa fursa kwa wadau kutoa maoni na kufanya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya elimu nchini, kwa njia ya mtandao na baadhi ya wadau kushiriki katika mkutano baada ya kukamilika kwa mpango wa pili  wa maendeleo ya sekta elimu ulioanzia mwaka 2017 na kukamilika Juni 31. 2021.

Akifunga mkutano huo, jijini Dar es Salaam leo Septemba 1. 2021 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, amesema baada ya kumalizika kwa mpango wa pili maandalizi ya mpango wa tatu wa maendeleo kwa miaka mitano mingine uanza kufanyika ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa hali halisi katika sekta ya elimu katika kipindi kilichopita.

Amesema katika mkutano huo wadau kwa pamoja wataangalia taarifa ya uchambuzi na kuangalia je yale yaliopangwa kufanyika yametekelezwa kwa kiasi gani, na ni chagamoto zipi zimeonekana na kipi kimesababisha kutokufikia malengo.

"Katika kipindi cha mpango uliopita tumefanya mambo mengi ambapo kwa upande wa miundombinu ya shule imeongezeka licha idadi ya wanafunzi kuongezwa kwa kasi kubwa kuliko matarajio,” amesema Dk. Akwilapo.

Amebainisha kuwa kwa sasa kuna idadi kubwa ya kuongezeka kwa wanafunzi kila mwaka hivyo serikali imekuwa ikiangalia namna bora itakayoleta mafanikio kwa nchi.

Dk. Akwilapo amesema kabla ya mkutano wa wadau timu ya wataalamu wa serikali na washauri elekezi uandaa andiko la awali ambalo uwasilishwa na kueleza kuwa mapendekezo utolewa katika taarifa ya uchambuzi wa sekta uzingatiwa wakati wa kuandaa mpango wa tatu wa sekta elimu awamu ya tatu.

Hata hivyo amesema zipo nyaraka mbalimbali ambazo uandaliwa na Serikali ambazo utumika kuandika mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu.

Nyaraka hizo ni mpango wa tatu wa miaka mitano ya maendeleo ya Taifa, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM,), Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na malengo ya maendeleo endelevu.

Aidha amesema maoni ya wadau ni ya muhimu sana kwani utoa fursa kwa wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kupanga mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mtaa TAMISEMI, Gerald Mweli amesema kila baada ya miaka mitano Serikali imekua ikiandaa mpango ili kuangalia ni namna gani itaweza kuboresha sekta elimu.

"Kabla ya kupata mpango mpya ambao utakuwa ni watatu tunafanya tathimini, chambuzi kujua hali elimu kwa ujumla"amesema Mweli.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili yapo mafanikio ambayo yamejitokeza ikiwa ni pamoja ujenzi wa miundombinu na madarasa kwa kipindi cha mwaka wa fedha na kuajiri walimu ili kuhakikisha ufundishaji unaendelea.

 Lydia Wilbard ni mmoja wa wadau walioshiriki katika mkutano huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) amesema ushiriki wao katika mkutano huo ni muhimu kwani wanapata fursa ya kutoa maoni na hatimaye kuweka mikakati bora kwa malengo Maalumu zaidi.

Amesema kupitia mkutano huo wanapata fursa ya kuangalia kwa undani sekta ya elimu na kusaidia kupanga mikakati maalumu itakayoweza kuleta matunda chanya katika kupata mkakati mpya.

No comments:

Post a Comment

Pages