September 25, 2021

MAPINDUZI YA VIVUKO NCHINI YANAVYOLETA NEEMA KWA WA NANCHI

Boti ya Uokoaji
MV Ilemela.
Mv Kazi.
Mv Pangani.
Mv Ukara.

Na Siti Said

Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ni Wakala wa Serikali ulioanzishwa chini ya Sheria ya Wakala Na.30 ya mwaka 1997 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 254 la tarehe 26 Agosti, 2005 na kuzinduliwa rasmi tarehe 23 Juni, 2006.

Wakala huu ulianzishwa kwa dhima ya kutoa huduma za uhakika, salama na zenye ubora wa hali ya juu katika fani za uhandisi mitambo, umeme na elektroniki, huduma za vivuko na ukodishaji mitambo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Aidha, Wakala huu unafanya majukumu mbalimbali ikiwemo kufanya matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali katika karakana ambazo zipo kila mkoa, kufanya matengenezo na usimikaji wa mifumo ya umeme, mabarafu, viyoyozi na Elektroniki inayomilikiwa na Serikali

Mbali na majukumu hayo,  pia Wakala unatoa ushauri wa kitaalam kwa Serikali na umma kuhusu masuala ya uendeshaji na usimamizi wa vivuko vya Serikali na kukodisha mitambo mbalimbali kama vile mitambo ya kuzalisha kokoto na mitambo ya kazi za barabara.

Kwa ufupi mbali na majukumu yote TEMESA iliyonayo bado inaendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuhahakisha inajituma kutekeleza majukumu yake ili kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla katika kazi za uendeshaji na ujenzi wa vivuko.

Mathalani, katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia vivuko kadhaa vimetengenezwa na vingine vikinunuliwa ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa majini katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Mfano wa maeneo hayo ni pamoja na Mwanza, Geita na Tanga.

Wananchi wa maeneo hayo wameshuhudia mapinduzi ya utoaji huduma za majini ambazo awali zilikuwa zinasusua kwa vipindi kadhaa kutokana na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu na uchakavu wa vivuko na hata kutokea kwa ajali katika kisiwa cha Ukara na kusababisha watu wengi kufariki na wengine kujeruhiwa pamoja na kivuko kuzama.

Katika kupambana na changamoto hizi, Wakala huu uliamua kujenga kivuko kipya cha MV Ukara II HAPA KAZI TU, MV Chato II HAPA KAZI TU pamoja na MV Pangani II kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za usafiri wa majini zinakuwa za uhakika na zinapatikana wakati wote.

Vilevile, Siku ya Tarehe 19 Oktoba, 2020, Serikali kupitia Wakala huu ilifanikiwa kurejesha tena faraja kwa wakazi wa visiwa vya Ukara na Bugorola mkoani Mwanza kwa kujenga kivuko cha MV UKARA II HAPA KAZI TU ambacho kilijengwa na Songoro Marine Transport ya jijini Mwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 ambacho kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 sawa na tani 100.

Ujenzi wa kivuko hiko ulikuwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli baada ya ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba, 2018, kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, aliagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya ununuzi wa Kivuko kipya na kikubwa kwa ajili ya Wananchi wa Ukara na Bugolora.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya wananchi kwa kuvikarabati na kununua vipya pale vinapohitajika kadiri uwezo wa Bajeti ya Serikali unavyoruhusu’’, alisema Mhandisi Kamwelwe .

Ujenzi wa kivuko cha MV.UKARA II ulianza mwezi Februari, 2019 lakini ulichelewa kukamilika kutokana na vifaa vilivyokuwa vimeagizwa kutoka nje ya nchi kuzuiwa kutokana na ugonjwa wa COVID – 19. Baada ya vifaa kuwasili Mkandarasi alifanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa kivuko hiki

Taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Maselle, kuhusu kivuko hiki inafafanua kuwa, kivuko hiki kina urefu wa mita 42 na upana wa mita 10 na kimefungwa injini mbili  ambazo zina uwezo mkubwa kwani  kinabeba abiria wengi zaidi tofauti na kivuko cha zamani (MV Nyerere) ambacho kilikuwa na uwezo wa kubeba tani 25 yaani abiria 101, magari 4 na mizigo.

 

Mhandisi Maselle, aliongeza kuwa kivuko hicho kinaendeshwa na mifumo mitatu ya usukani (steering) moja kati ya hizo ni Hydraullics, Electro-Hydraullic na (emergency steering system) kimejengwa kwa kutumia mabati maalumu (grade A marine plate) yanayotumika kujengea vyombo vya usafiri wa majini.

 

Kwa upande wa Kivuko cha Mv Chato II HAPA KAZI TU ambacho pia kimejengwa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini Mwanza kilichogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.1 ambacho kinatoa huduma zake za usafirishaji kati ya Chato Muharamba na Nkome mkoani Geita. Kivuko hiki kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari madogo 10 sawa na tani 100.

Mbali na ujenzi wa vivuko hivi,  pia Serikali ilikifanyia ukarabati mkubwa kivuko cha MV.PANGANI II ambacho kilipokewa Tarehe 21 Oktoba, 2020 Wilayani Pangani mkoani Tanga. 

Ukarabati wa kivuko hiki umegharimu shilingi milioni 496 ambapo kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari madogo 4 sawa na tani 50 na kutoa huduma kati ya Pangani na Bweni Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, inayohusu Muundo na majukumu ya Wakala iliyowasilishwa  tarehe 26 Januari, 2021  Bungeni jijini Dodoma, katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ambayo ilieleza kuwa kuna miradi kadhaa ya ukarabati wa vivuko ambayo imepangwa kufanywa kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambapo kiasi cha shilingi Bilioni Nne kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema kuwa Wakala umeanza na mradi wa ukarabati wa kivuko cha MV Tegemeo, ambapo mradi wa ukarabati wa MV Musoma na MV Mara unasubiri upatikanaji wa fedha.

Aliongeza kuwa Ukarabati wa Boti ya Uokozi ya MV KIU na MV Sengerema bado unaendelea wakati ukarabati wa mradi wa Mv Ujenzi upo katika hatua ya kusaini mkataba. Amefafanua kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaenda sambamba na ujenzi wa maegesho yake kwa kuwa huwezi kuwa na vivuko bora wakati maegesho hayana mbele wala nyuma.

Kwa kulizingatia hilo, Wakala kwa mwaka wa fedha 2020/21 pia ulitenga kiasi cha shilingi Biloni Mbili  ambazo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo upanuzi wa Jengo la abiria katika Kivuko cha Magogoni – kigamboni ambapo upande wa Kigamboni jengo limekamilika na kazi inayoendelea kwa sasa ni usimikaji wa miundombinu ya umeme na mashine za kukatia tiketi.

Pia ujenzi wa maegesho ya Bukondo na Zumacheli katika kivuko cha Chato- Nkome ambapo maegesho ya Bukondo yamekamilika na ujenzi wa maegesho ya Zumacheli utaanza baada ya kupatikana kwa fedha.

Ujenzi na ukarabati wa maegesho ya vivuko Nane vya Bugolora- Ukara, Rugezi- Kisorya, Kilambo- Namoto, Utete- Mkongo, Iramba- Majita, Nyakaliro- kome, Kasharau- Buganguzi na Musoma- Kinesi.

Maboresho na ukarabati wa miundombinu hiyo unaenda sambamba na Ujenzi wa miundombinu ya jengo la abiria, chumba cha kukatia tiketi, ofisi na uzio katika kivuko cha Kayenze – Bezi na Itungi Port Mbeya ambapo jengo la abiria upande wa Kayenze limekamilika na upande wa bezi na Itungi Port, Mbeya ujenzi unaendelea.

Kutokana na makala hii utaona ni jinsi gani Serikali kupitia Wakala huu ilivyofanya jitihada kubwa kuhakikisha maendeleo na huduma za usafiri na usafirishaji zinafika kwa wananchi kwa namna moja ama nyingine na kupelekea kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali.

 

No comments:

Post a Comment

Pages