September 04, 2021

Mwigulu aziagiza halmashauri kulipa madeni

Regina Frank, Sandra Charles na Rahma Taratibu, (SJMC), Dodoma.


HALMASHAURI zote nchini zimeagizwa kuhakikisha zinalipa madeni yote ya watoa huduma ndani ya miezi mitatu kabla ya kumalizika kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 mwezi Septemba mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu marekebisho ya tozo ya Miamala ya simu baada ya kusaini marekebisho ya Kanuni hizo .

“Mheshimiwa Rais anaguswa sana na madeni ya watoa huduma hasa watoa huduma wadogo, fedha zao kukaa Serikalini kwa muda mrefu, wengine walikopa kwenye mabenki na wengine wameshapata misukosuko, Mheshimiwa Rais ameagiza walipwe haraka”, amesema.

Nchemba amesema kuwa watoa huduma hao walipwe haraka ili fedha hizo ziingie kwenye mzunguko kwa kuwa kutokuwalipa ni sawa na kuwatia umasikini kitu ambacho si lengo la Serikali.

Kuhusu Tozo za Miamala ya Simu,  Nchemba amesema mpaka tarehe 31 Agosti 2021 Serikali imekusanya jumla ya Sh. bilioni 63 ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya 220 katika Tarafa zote 220 ambazo hazijawahi kuwa na huduma hiyo tangu nchi ipate uhuru.

Amesema fedha zitakazokusanywa kutoka katika tozo hizo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kununua madawati ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

“Januari mwakani tutaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotarajiwa kuongezeka mara mbili ya mwaka uliopita, si vema tukarudi kule tulikotoka kwa wanafunzi kufaulu 50 halafu anachaguliwa mmoja kutokana na ukosefu wa madarasa”, amefafanua.

Nchemba  amesema kwa ruhusa aliyopewa na Waziri wa Nchi TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu, amewaagiza Madiwani kutoa taarifa rasmi ya mahitaji ya Madarasa kwa kila Kata kwa ajili ya Wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Amesema taarifa hizo zitaiwezesha Serikali kugawa fedha kutokana na mahitaji ili kuhakikisha azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inayotaka wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa darasa la saba watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanadahiliwa.


Waziri Wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, akijibu swali wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ufafanuzi wa marekebisho ya kanuni za tozo za miamala ya simu, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma, kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Benny Mwaipaja.

No comments:

Post a Comment

Pages