September 14, 2021

Rais Samia mgeni rasmi Tamasha la Michezo la Tanzanite

 

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo (BMT) Neema Msitha akizungumza na wanahabari kuhusu Tamasha la Michezo la Tanzanite litakalofanyika kuanzia Septemba 16-18 mwaka katika Viwanja vya Benjamin Mkapa.

 

Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Michezo kwa Wanawake 'Tamasha la Michezo la Tanzanite litakalofanyika Viwanja vya Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 16  hadi Septemba 18 mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbas, Kaimu Katibu  Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo Neema Msitha amesema siku ya kwanza ya tamasha kutakuwa na kongamano la kujadil michezo na kwamba mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wabobezi.

“Hali halisi kuelekea kwenye tamasha letu iko vizuri, tunawakaribisha sana wanawake wote wa Dar es salaam na wamikoani pia mje mnufaike na mambo mazuri na mengi ya wanawake,’’amesema Msitha.

Amezitaja baadhi ya mada hizo ni uhalisi wa wanawake katika kushiriki michezo,  maadili na taaluma ya michezo kwa wanawake pamoja na mchango wa vyombo vya habari katika michezo.

Msitha amesemaTarehe 17 tamasha litapambwa na michezo nane ya wanawake kutoka katika timu vinara za taifa zikiwemo ngumi za wazi na kulipwa, Wanariadha kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Mpira wa Netibali utakaoshindanisha timu ya JKT Mbweni na Uhamiaji, Mpira wa miguu kati ya timu ya Simba Queen na timu ya Taifa ya U 20, Mpira wa wavu kati ya timu ya Jeshi stars na Magereza, Mpira wa kikapu kati ya timu ya Don Bosco na JKT pamoja na timu ya watu wenye ulemavu kwa mpira wa kikapu.

 Amesisitiza kuwa vilabu vya michezo hiyo vimethibitisha kushiriki na kwamba siku ya tatu ya mashindano hayo michezo itamaliziwa kwa washidi kupewa zawadi na kwamba mgeni rasmi atakuwa Rais Samia.

Ameongeza kuwa lengo ni kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ambaye katika hotuba zake ameonekana mafanikio ya timu za wanawake lakini hazitangazwi kama za wanaume pamoja na kuhamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo kwani michezo ni ajira na hujenga afya.

No comments:

Post a Comment

Pages