September 30, 2021

Wananchi wapewe elimu kuhusu Chanjo

 Na Lydia LugakilaMuleba


Serikali wilayani Muleba mkoani Kagera imedhamilia  kuhakikisha ifikapo Oktoba 3, mwaka huu iwe imeishamaliza dozi ya chanjo ya uviko 19 ya aina ya Johnson Johnson katika vituo vyote vya kutolea huduma ya afya badala ya Oktoba 05 mwaka huu kama ilivyo matarajio ya serikali.

Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa chanjo Wilaya ya Muleba Bi. Christina Mremi katika ufunguzi wa kikao cha kamati ya afya ya msingi ambapo amesema kuwa Wilaya hiyo ilipokea jumla ya dozi ya chanjo ya UVICO 7,000 na hadi sasa zimeishatumika dozi 2,440 sawa na asilimia 34.86.

Bi. Mremi amesema kuwa hadi sasa ipo jumla ya dozi 4,560  sawa na asilimia 65.14 ambapo chanjo hiyo inatolewa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma ya afya 45 badala ya 3 kama ilivyokuwa awali lengo ikiwa ni kuhakikisha ifikapo Oktoba 03 dozi hiyo iwe imeishamalizika.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila ameagiza kila zahanati ichanje jumla ya watu 20 kila siku na kituo cha afya watu 25 kwa siku pamoja na watu 30 kwenye hospitali tatu zote ziliopo wilayani humo na kila siku awe anapata taarifa ya watu hao waliopata chanjo.

Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameshauri watoa huduma ya chanjo kutowalazimisha wananchi kuchanja bali wahamasishwe pamoja na kupatiwa elimu ya kuchanja kwa hiari kwa kila taasisi mbalimbali ili kuweza kufikia lengo la serikali na kusaidia jamii iweze kujikinga na ugonjwa wa uvico 19.

No comments:

Post a Comment

Pages