Mkurugenzi Mkuu NHIF, Benard Kongwa.
SERIKALI imewataka watoa huduma za matibabu kuonesha utofauti katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ili kuwavutia wananchi wengine ambao wako nje ya mfumo wa bima ya afya.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Hassan Rugwa wakati akifungua mkutano kati ya NHIF na Watoa Huduma wote nchini ambao ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya utoaji wa huduma kwa wanachama wa Mfuko na maboresho yaliyofanyika ndani ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo.
“Tujipange kuanzia kwa wahudumu wetu wa afya kutoa huduma bora hadi kwenye kuimarisha mazingira ya vituo vyetu, Serikali yetu imeshawekeza kwa kujenga vituo vyenye mazingira mazuri mpaka ngazi za chini na inaendelea kuongeza bajeti ya afya kuhakikisha miundombinu na rasilimali watu zinatosheleza katika kutoa huduma bora hivyo ni kila mmoja aoneshe utofauti kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na wanachama wa Mfuko,” alisema Bw. Rugwa.
Alisema kuwa hakuna sababu ya kuwa na huduma mbaya kwa sasa kutokana na nguvu kubwa ya Serikali iliyoelekezwa katika uimarishaji na upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika vituo vyote vya Serikali na kwamba wakati umefika kwa Watoa huduma wote wa Serikali kuonesha umakini katika usimamiaji na utoaji wa huduma.
Aliupongeza Mfuko kwa kazi kubwa ambayo imefanyika katika kuimarisha mifumo ya TEHAMA ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma kwa upande wa wanachama na watoa huduma katika ulipwaji wa malipo yao.
“Nipongeze NHIF na Watoa huduma ambao wameweza kuunganisha mifumo yao na kurahisisha kwa kiasi kikubwa ushughulikiaji wa malipo ya madai, niwaombe sana vituo ambavyo bado hamjaunganisha mfumo wenu na NHIF mfanye hivyo ili muweze kulipwa kwa wakati,” alisema Bw. Rugwa.
Katika hatua nyingine alikemea vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na kuwataka kuacha mara moja na badala yake kila mmoja awajibike katika kuulinda Mfuko ili uwe imara na uendelee kuhudumia watanzania wa sasa na vizazi vijavyo.
“Niwaombe sana NHIF kudumisha mahusiano na Watoa huduma wanaohudumia wanachama katika kukabiliana na suala hili, vikiwepo viashiria vya udanganyifu basi pande zote mbili zikae kwa uwazi na kuziainisha ili kuona kwa pamoja na kuchukua hatua inayostahili,” alisema.
Akizungumzia safari ya NHIF ya miaka 20, aliupongeza Mfuko kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa yakiwemo ya uboreshaji wa huduma na namna Mfuko ulivyoshiriki katika uimarishaji wa huduma za matibabu katika vituo mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa ndani ya miaka 20, amesema kuwa, Mfuko umeshiriki moja kwa moja katika uimarishaji wa huduma kupitia mikopo nafuu ya uboreshaji wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba na dawa.
Kwa upande wa huduma, alisema NHIF imeimarisha utendaji kazi wake kupitia uwekezaji uliofanyika katika eneo la TEHAMA hatua iliyosaidia kwa kiwango kikubwa katika upatikanaji wa huduma kwa uharaka zaidi na kuwatambua wanachama wakati wa kupata huduma za matibabu.
“Mifumo imetusaidia sana katika meeneo mengi likiwemo la ulipaji wa madai ambapo kwa sasa tumeweza kulipa vituo vilivyounganishwa na mfumo kwa siku 14 na kupitia mifumo hii tunaamini tutaondokana na changamoto ya ucheleweshaji wa madai ambao umekuwa ukileta usumbufu usiokuwa na tija,” alisema Bw. Konga.
Aidha amesema, eneo jingine ni maboresho yaliyofanyika katika kitita cha mafao ambapo kwa sasa wanachama wanapata huduma nyingi zikiwemo za kitaalam zaidi tofauti na ilivyokuwa awali. “Tumefanikiwa kuwa na mtandao mkubwa wa vituo vya kutolea huduma za matibabu kutoka vituo 3,000 hadi zaidi ya vituo 8,000 kwa sasa haya ni mafanikio makubwa kwetu,” alisema Bw. Konga.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF Bw. Juma Muhimbi amewahakikishia watoa huduma hao kuwa Mfuko utaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia hali ya Mfuko pamoja na mahitaji yaliyopo. Ameanisha Bodi imejipanga kisimamia utekelezaji wa mambo yote ya msingi kwa maendeleo ya Mfuko na suala la afya nchini.
No comments:
Post a Comment