September 06, 2021

Waziri Mkuu Majaliwa azindua NMB Foundation


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa tatu kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna wakizindua Asasi ya NMB Foundation yenye lengo la kuwekeza zaidi kwenye sekta ya elimu, mazingira, afya, kilimo na ujasiriamali, hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dk. Edwin Mhede. (Na Mpiga Picha Wetu).  


NA MWANDISHI WETU


BENKI ya NMB imezindua asasi ya kiraia iitwayo NMB Foundation, inayolenga kujikita katika kuimarisha uwekezaji wake kwa jamii katika sekta tano teule, sambamba na Mpango Maalum wa Udhamini wa Masomo 'NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship,' uzinduzi uliohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kupitia NMB Foundation, benki hiyo inaunga mkono zaidi jitihada za Serikali kuimarisha maendeleo, ambako inaenda kuvuka mipaka ya Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambayo kwa miaka 16 ya uwepo wake, imetumia zaidi ya Sh. Bilioni 12 za urejeshaji kwa jamii kupitia asilimia moja ya faida yake kila mwaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB (CEO), Ruth Zaipuna, alisema asasi hiyo imejipanga kuacha alama kwa jamii ya Kitanzania, kupitia uwekezaji na urejeshaji kwa jamii kwenye sekta tano za kipaumbele ambazo ni elimu, afya, kilimo, mazingira na ujasiriamali.

Akichanganua majukumu ya NMB Foundation, Zaipuna alisema katika elimu wanatarajia kutoa misaada zaidi ya ilivyokuwa ikifanya kupitia CSR, ambako itajielekeza kukuza elimu na kuongeza idadi ya watoto wanaopata elimu, huku kwenye afya ikilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalum na jamii kwa ujumla.

"Kwa upande wa mazingira, tunakusudia kuhamasisha utunzaji wake kwa lengo la kuboresha makazi ya jamii, wakati kwenye kilimo nia ni kuimarisha uwezo wa vyama vya ushirika na kuwaongezea ujuzi kupitia elimu na mafunzo ya masuala ya fedha, biashara na kuwajengea wakulima uwezo wa kukopesheka.

"Katika ujasiriamali, NMB Foundation itahakikisha inafanikisha juhudi za uzalishaji na utoaji ajira, lakini pia kukuza uchumi kwa kutoa mafunzo na uwezeshaji wa elimu ya fedha, matumizi ya dijitali, ubunifu na uendelezaji wa biashara ili kuharakisha mabadiliko chanya katika sekta hiyo, inayokusanya Kundi kubwa la vijana," alisisitiza Zaipuna.

Kupitia 'NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship,' Zaipuna alifafanua kuwa Ni program ya ufadhili wa masomo kwa vijana wa ngazi ya chuo na Sekondari wanaotoka katika familia zisizojiweza, ambao utaanzia mwaka huu wa masomo wa 2021/22, wanakoratarajia kusaidia vijana 200, wakiwamo wanachuo wa shahada ya kwanza 50 na wanafunzi wa Sekondari 150 kote nchini.

Kabla ya kuzindua NMB Foundation na NMB Nuru Yangu Scholarship, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliipongeza NMB kwa ubunifu uliozaa asasi na program zilizozinduliwa, ambazo ni rafiki kwa jamii, zinazoenda moja kwa moja kusapoti jitihada za Serikali katika kusimamia maeneo yote yaliyotajwa katika vipaumbele vitano vilivyoainishwa.

Alibainisha kuwa, NMB sio wageni wa kuunga mkono jitihada za Serikali kutatua changamoto za kijamii na kwamba NMB Foundation na NMB Nuru Yangu, ni kielelezo cha benki inavyojitoa katika kuitendea haki jamii ya Watanzania na kuwa kupitia CSR, kwa miaka mitano iliyopita benki hiyo imeweza kuwafikia wanufaika zaidi ya milioni 5 kote nchini.

"UZINDUZI huu unaofanyika hapa una baraka zote za Serikali, kwa sababu tunatambua kuwa asasi hii ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Taifa na watu wake, kama ilivyo pia kwa Programu ya NMB Nuru Yangu, ambayo inaenda kuwabeba mamia ya vijana wetu kutoka katika jamii ya wasiojiweza, ambao sisi Kama Serikali tayari tumeshawekeza vya kutosha katika kuwakomboa kielimu.

"Serikali tunaahidi sapoti ya kila namna kwa NMB kutokana na jinsi inavyojitoa katika kutuunga mkono kwenye maeneo mbalimbali. 

"Mchango wa NMB kwa jamii ni mkubwa unaopaswa kuigwa na wadau wengine. Serikali inatambua na kuthamini harakati chanya za benki hii, tunawaomba endeleeni kuchapa kazi, tuko nyuma yenu," alisisitiza Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment

Pages