October 10, 2021

ACT: Ni ushindi halali Konde


Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde, Mohamed Said Issa.


Na Mwandishi Wetu, Pemba

Chama Cha ACT Wazalendo kinawapongeza na kuwashukuru viongozi , wanachama na wananchi wa Jimbo la Konde kwa ushindi mkubwa wa halali ambao chama kimeupata kwenye Uchaguzi wa marudio uliofanyika jana Oktoba 9, 2021.

Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Khatib. Said Haji.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Salim Biman leo, Oktoba 10, 2021 imesema ushindi huo umepatikana kutokana na kuwepo usimamizi mzuri kwa mujibu wa sheria na kuheshimu matakwa ya wananchi wa Konde.

"Tunachukua fursa hii pia kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kuheshimu matakwa ya Wananchi wa Konde. Tunaipongeza pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha Uchaguzi unafanyika kwenye hali ya amani na utulivu." Amesema Bimani katika taarifa yake.

Aidha katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo,  Ado Shaibu Ado anatarajiwa kufanya uchambuzi wa kina wa mwenendo wa Uchaguzi kwenye Majimbo na kata mbalimbali chini na kutoa mwelekeo wa chama kuhusu suala hilo.
Katika uchaguzi huo, ACT Wazalendo kimepata kura 2391 dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoambulia kura 794, CUF kura 98 huku chama cha AFP kikipata kura 55.

No comments:

Post a Comment

Pages