October 04, 2021

MAJALIWA: SERIKALI IMEDHAMIRIA KUTEKELEZA DHANA YA UCHUMI JUMUISHI KWA VITENDO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutekeleza dhana ya uchumi jumuishi kwa vitendo kwa kuweka vipaumbele vitakavyowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 4, 2021) wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tano la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, jijini Dodoma. Amesema kuwa vipaumbele katika mipango ya Serikali vimekuwa katika utekelezaji wa shughuli za kiuchumi zinazowajumuisha moja kwa moja wananchi.

Waziri Mkuu ametaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na uimarishaji wa huduma za afya, hifadhi ya jamii, maji, umeme na utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila ada “Mtanzania mwenye afya, aliyeelimika na miundombinu wezeshi ni chachu kwa ukuaji uchumi wa nchi yetu.”

Amesema uwezeshaji wa uchumi jumuishi ni msingi wa kuhakikisha kunakuwa na ustawi endelevu kwa watu wote, ambapo Serikali imeandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambayo pamoja na mambo mengine imeainisha mazingira wezeshi yatakayowezesha nchi kunufaika kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pia imelenga kuhakikisha kunakuwa na viwango vya juu vya maisha, amani na umoja, utawala bora na uchumi ulioimarika wenye ushindani katika jamii.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa sera mbalimbali ambazo zimelenga kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu na uchumi jumuishi. “Kati ya Sera hizo ni Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo ni Sera kiongozi kwenye masuala ya kuwezesha wananchi kiuchumi, sera hiyo imeweka mikakati inayolenga kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa maagizo kwa viongozi wa wizara, mikoa, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa masuala ya uwezeshaji wahakikishe dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuiwezesha nchi kuwa na uchumi jumuishi itimie.

“Anzisheni vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, ambavyo vitatoa huduma za mikopo, mafunzo, urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za masoko na kutoa ithibati ya bidhaa zinazozalishwa kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020”

Ameongeza kuwa viongozi wa mikoa wasimamie uimarishwaji wa majukwaa ya wanawake kwenye mikoa kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais Samia alipokutana na wanawake Jijini Dodoma tarehe 8 Juni, 2021.

“Taasisi za umma na binafsi zinazosimamia mifuko na programu za uwezeshaji zinazotoa mitaji na ruzuku zihakikishe kuwa zinaweka watumishi kwenye vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili uwepo wa vituo hivyo uwe na maana kwa wananchi wanaokwenda kupata huduma na ziimarishe huduma ili kuwezesha ustawi na kukua kwa uchumi wa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni kwa lengo la kupunguza umaskini na kuchochea shughuli za kiuchumi.”

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Viwanda na Baishara, SIDO, VETA pamoja na taasisi za elimu za umma na binafsi zitoe mafunzo na ujuzi kwa Watanzania kulingana na mahitaji ya soko la Kitaifa na Kimataifa ili wananchi waweze kuzalisha bidhaa bora na kutoa huduma zenye viwango zinazoweza kuhimili ushindani ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza halmashauri zote ziweke mazingira wezeshi na ziendelee kutenge maeneo maalumu yatakayowawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kukua, kustawi na kufanya shughuli za kiuchumi.

“Halmashauri zote nchini zihakikishe afua za uwezeshaji wananchi zinatengewa bajeti na kuwajengea uwezo Maafisa Biashara ili waweze kuratibu kwa ufanisi masuala ya uwezeshaji katika halmashauri zao.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezindua Kanzidata ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo ipo chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikiwa na lengo la kuwaunganisha watoa huduma wa kitanzania na wawekezaji pamoja na taasisi mbalimbali za uwezeshaji.

Ni matarajio yangu kwamba Kanzidata hii itaongeza ushiriki wa watanzania kwa kuwa itawawezesha kujulikana, kufahamu fursa kwenye miradi mbalimbali na kutambua wadau ambao wanaweza kushirikiana na kuingia ubia ili kupata fursa mbalimbali kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa nchini.”

Ninaomba nitumie fursa hii, kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia kwa dhamiri yake kubwa aliyoonesha katika kukuza uwezeshaji kwa wananchi hasa wanawake, vijana, wafanyabiashara, wajasiriamali na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geoffrey Mwambe amewaagiza wakuu wa mikoa wasimamie ipasavyo shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi katika maeneo yao zinakuwa na tija ili kuhakikisha malengo ya Mheshimiwa Rais Samia yanafikiwa.

Waziri Mwambe amesema kwamba kongamano la uwezeshaji wananchi kiuchumi lilianzishwa mwaka 2015/2016 ili kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji kwa lengo la kujadili na kupeana uzoefu katika kuwawezesha watanzania.

Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa alisema baraza hilo limeendelea kuratibu na kusimamia mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo kwa kushirikiana na ile inayotoa dhamana imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 4.97 kwa wajasiriamali 7,231,617.

Alisema Baraza hilo limesimamia uanzishwaji wa vituo vya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi katika mikoa mbalimbali ambapo kwa sasa vimefikia 17 katika mikoa sita ya Geita, Shinyanga, Singida, Rukwa, Dodoma na Kigoma ambavyo katika kipindi cha mwaka mmoja vimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 24 kwa wafanyabiashara 3,233 na mafunzo ya ujuzi na biashara kwa watu 1,990.

No comments:

Post a Comment

Pages