October 07, 2021

NMB yatenga Bil 100/- kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kukopa kwa riba isiyozidi %10


Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa mikopo ya riba nafuu kwa wateja katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo zaidi ya Sh. Bilioni 100 zimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara, Isaac Masusu.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi,  akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikopo ya riba nafuu kwa wateja katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ambapo zaidi ya Sh. Bilioni 100 zimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo. Hafla hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni  Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara, Isaac Masusu.

 

Na Mwandishi Wetu

 

 

BENKI ya NMB imetenga Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali waliopo katika mnyororo wa thamani wa wakulima, wafugaji na wavuvi.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna alisema mkopo huo wenye riba nafuu isiyozidi asilimia 10 niwa kipekee ambao utaanza rasmi mnamo Oktoba 15 mwaka huu.

 

“Tumeweka kuwa na kiwango cha kukopa kuanzia Shilingi 200,000 hadi Shilingi Bilioni 1, ambapo wanaruhusiwa kukopa mtu mmoja mmoja, kikundi, taasisi, mashirika na vyama vya ushirika kwa kufuata masharti ya mikopo inayojulikana,” alisema Bi. Zaipuna.

 

Alibainisha kuwa wameamua kuja na mkopo huo wa kipekee kwa kuwa wanataka kuhakikisha wajasiriamali waliopo katika mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi wananufaika kiuchumi kutokana na mitaji ya uhakika.

 

“Benki ya NMB inachukua hatua hii ili kupanua wigo wa wadau wengi katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itaongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.

 

“Ni matarajio ya benki ya NMB kuwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati katika tasnia hii wataitumia fursa hii adhimu kujipatia mikopo yenye gharama nafuu na kujiongezea kipato ili kujenga uchumi wa nchi,” alisema Bi. Zaipuna.

 

Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi alisema hii si mara ya kwanza kwa benki ya NMB kuja na mpango wa kuwasaidia wakulima, benki hiyo imekuwa na utamaduni wa kusaidia wajasiriamali katika nyanja mbalimbali kwa kipindi kirefu.

 

“Sisi (Benki ya NMB) kwa mwezi tunatoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 50 kwa wajasiriamali wa viwango mbalimbali, masharti tunayoweka ni yale yanayotambulika na wateja wetu pamoja na Watanzania wote, si magumu na rahisi kufikiwa,” alisema Mponzi.

 

Katika hatua nyingine Bi Ruth Zaipuna akizungumzia suala la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutenga fedha zaidi ya Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya wakulima, alisema mpango wa Benki ya NMB kuja na utaratibu huu ni wao hauhusiani na utaratibu wa BoT, lakini wataangalia namna ya kuongezea kwenye utaratibu walio nao. 

 

“Hili ni la kwetu NMB, tukiwa na lengo la kuwasaidia wananchi, lakini fursa iliyotangazwa na BoT tutaitumia pia kwa ajili ya kuwanufaisha zaidi wateja wetu. Hii Shilingi Bilioni 100 tuliyoiweka haina muda maalumu, ikiisha tutafany tathmini ikiwezekana tutaiongeza.

 

“Ikumbukwe hadi sasa Benki ya NMB kwa upande wa sekta ya kilimo pekee tumeshatoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.1. ndani ya maika mitano kwa hiyo mtaelewa kuwa hili si suala geni kwa wateja wetu. Vilevile suala la mabadiliko ya tabianchi tunalitambua, ieleweke lolote litakalotokea hiyo ni hatari kama zilivyo hatari nyingine kwenye uwekezaji, ndiyo maana kuna utaratibu wa kuikatia bima mikopo yetu,” alifafanua Bi. Zaipuna. 

 

Kutokana na mkopo huo taifa litaongeza uzalishaji wa chakula, malighafi za viwanda na kuchagiza maendeleo ya viwanda nchini, ambapo benki hiyo inatoa wito kwa walengwa kuwasiliana na mtandao wake wa zaidi ya matawi 225 yaliyo enea nchi nzima ili kuweza kupata huduma za mikopo hii ya riba nafuu.

No comments:

Post a Comment

Pages