Hayo ameyasema jijini humo alipotembelea ujenzi wa nyumba hizo zilizopo eneo la Magomeni na kusema kuwa ujenzi wa nyumba hizo umekamilika kwa asilimia 100 hivyo wakazi watakaohamia wanatakiwa kutunza miundombinu.
Amebainisha kuwa wakazi hao wanapopata fursa ya kuingia kwenye nyumba hizo Serikali haitaki kuona ndani ya mwaka mmoja kila kitu kimevurugika huku zikiharibiwa kwani Serikali inataka kuendelea kuboresha makazi ya wananchi nchini.
"Tunawaomba mtakapokabidhiwa nyumba hizi mjitahidi kuzitunza bahati nzuri miundombinu yote ipo vizuri na yanaweza kutimiza malengo ya wakazi watakaokaa hapa. Wakati wowote mradi huu utafunguliwa na michakato imeshafanyika mingi na wakazi 644 wametambuliwa ni nani ataingia wapi na taratibu zote zinakamilika," amesema Balozi Amour.
Amesisitiza kuwa kazi kubwa imeshakamilika kwa asilimia 100 kilichobaki taratibu za ujenzi wa marekebisho na maboresho madogo madogo ambayo yanaendelea.
Amour ameongeza kuwa kuna mipango mingine inaendelea kama ya aina ya mradi huo kwa sababu ni mara yao ya kwanza mradi huo kutekelezeka kwa kiwango cha ubora hivyo wakazi hao wasaidie kuitunza miundombinu ya nyumba hizo ili fedha za serikali ziweze kufanya kazi nyingine
Pia amesema katika mradi huo wamefikiria tatizo kubwa la Wamachinga hivyo wamejenga eneo linaloitwa 'Wamachinga Center’ ambalo watafanyia biashara hivyo wameombwa watakaofanya biashara watumie eneo hilo kwa matumizi yaliyopangwa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro amesema mradi huo umekamilika hivyo wakazi 644 watakaa kwenye nyumba hizo.
"Wakazi wa nyumba 644 wote wataingia kwenye nyumba hizo na tuna maeneo ya uwekezaji ambalo ni Machinga Center ambalo lina vizimba 286, vyoo vya kulipia na uwekezaji wa sakafu juu na chini," amesema Kondoro.
Naye Mwenyekiti wa Wakazi wa Magomeni, George Abel amesema wanaishukuru Serikali kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba hizo na kuiomba kuwapa mkataba wa kuingia ndani huku akifafanua kuwa inafahamika nyumba hizo zitauzwa kwa bei nafuu.
No comments:
Post a Comment