Msimamizi wa Kituo cha Kutolea Huduma kwa Wateja cha Ofisi ya Rais -TAMISEMI Antelma Mtemahanji (kushoto), akimuelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa aliyevaa suti za kijivu namna kituo hicho konavyofanya kazi.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amesema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa Kituo cha Kutolea Huduma kwa Wateja cha Ofisi ya Rais –TAMISEMI.
Pia amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kuweka mikakati ya uanzishwaji wa Kituo cha kutolea huduma kwa mteja kwa kila Mkoa ili kurahisisha utoaji wa Huduma bora kwa wananchi.
Agizo hilo amelitoa leo Januari 18 2022, jijini Dodoma alipotembelea Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa lengo la kuangalia maelekezo aliyoyatoa awali kuhusu maboresho ya kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa wananchi.
Bashungwa amesema ingekuwa vyema vituo hivyo vingekuwa vinapatikana katika ngazi ya Mikoa ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka tofauti na ilivyo sasa hadi wapige simu Wizarani kutatuliwa kero za.
" Tunawajibu wa kuweka mikakati ya kushusha huduma hizo mikoani lengo likiwa ni kuwapunguzia adha wananchi kufuata huduma ngazi ya Wizara, " amesema Waziri Bashungwa.
Pia Waziri Bashungwa amemuagiza katibu Mkuu huyo kuhakikisha anatafuta rasilimali fedha na vifaa ili kuhakikisha ule mkakati wa kuweka nguvu na kuimarisha Sekretarieti za Mikoa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, Tarafa , Wilaya na Mkoa unafanikiwa.
Waziri Bashungwa amesema Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ndio watakaokuwa wasimamizi wakuu wa vituo hivyo vya kutolea Huduma kwa wateja lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora inapelekwa kwa wananchi katika maeneo yao na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma Wiazarani.
Mbali na huduma hiyo Waziri Bashungwa ameongeza kuwa amepokea simu nyingi kutoka kqa wazazi, walezi wakimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa madarasa bora yaliyotokana na fedha za mradi wa UVIKO-19.
“Jambo hili limeanza vizuri ngazi ya Wizara, hivyo tuimarishe kwenye Mikoa ili kuweza kuwasaidia wananchi. Nawaagiza kuhakikisha tunaweka mikakati ya kila Mkoa kuwa na Kituo cha Huduma kwa wateja ili wananchi wanapohitaji huduma kutoka Mikoani wanakuwa na namba ambazo wanaweza kupiga badala ya kutoka Vijijini kuja kupata huduma Wizarani.” Amesisitiza Waziri Bashungwa
Naye Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja Antelma Mtemahanji amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuwasaidia wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutoka vijijini hadi kufika Ofisi ya Rais –TAMISEMI kufuata huduma mbalimbali za kiofisi.
Amesema tangu kituo kimeanzishwa mwaka 2020 hadi sasa simu 125, 381 zilizopokelewa na kufanyiwa kazi katika kituo hicho.
Aidha,amesema kabla ya kuanzishwa kwa kituo hicho Ofisi ya Rais –TAMISEMI ilikuwa ikipokea wateja 100 hadi 120 kwa siku ambao walikuwa wakifika ofisini kufuata huduma na kwamba kwa sasa hali hiyo imepungua na kupunguza mlundikano wa wananchi kufuata huduma Wizarani.

No comments:
Post a Comment