January 24, 2022

NMB, SMZ kushirikiana sekta ya utalii


Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Fatma Mbarouk Khamis (wa pili kulia) akibadilishana mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Wizara hiyo na Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja binafsi NMB,Filibert Mponzi, wakatiwa hafla fupi ya kusainiana mkataba huo iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo mjini Zanzibar. Wa pili kushoto ni Meneja wa Tawi la NMB na Kaimu Meneja wa Biashara NMB Zanzibar, Naima Shaame. Kushoto ni Mkuu wa Biashara ya Kadi NMB Zanzibar, Philbert Casmir na kulia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hafsa Mbamba. (Na Mpiga Picha Wetu).

Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja binafsi NMB, Filibert Mponzi, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo mjini Zanzibar jana, Januari 21/2022. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Mbarouk Khamis (kushoto) ni Mkuu wa Biashara ya Kadi NMB Zanzibar, Philbert Casmir.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Fatma Mbarouk Khamis (wa tatu kutoka kulia), Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja binafsi NMB, Filibert Mponzi (wa tatu kutoka kushoto) wakisainiana mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Wizara hiyo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo mjini Zanzibar. Wa pili(kushoto) ni Mwanasheria wa NMB, Herbert Clipa (wa pili kulia) ni Mwanasheria wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Mustafa Omary Abdallah. (kushoto) ni Mkuu wa Biashara ya Kadi NMB Zanzibar, Philbert Casmir (kulia) ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hafsa Mbamba.

 

Na Mwandishi Wetu

 

WIZARA ya Utalii na Mambo ya Kale Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati ya kushirikiana na Benki ya NMB kutoa mafunzo kwa vijana wanaotembeza watalii ili kurasimisha shughuli zao waweze kukopesheka.

Hayo yameelezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Fatma Mabrouk Khamis wakati wa kutiliana saini makubaliano kati ya wizara hiyo na Benki ya NMB kuinua shughuli za utalii visiwani humo.

 Akizungumza wakati wa mkutano huo uliofanyika jana visiwani Zanzibar, Bi. Fatma Mabrouk Khamis alisema kuna kundi kubwa la vijana wanaozagaa mitaani bila ujuzi wa kuongoza watalii, ambao wanaharibu taswir ya visiwa hivyo, ambapo wakipewa mafunzo na kurasimishwa itawasaidia kiuchumi na kijamii.

“Vijana wanaojihusisha na utalii mfano beach boys ambao maranyingi wanakuwa kero kwa wageni, wanafanya utalii wa mikobani. Kwa kushirikiana na NMB tutawakusanya tutawapa mafunzo na kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kuwaunga na jumuiya ili kuwahusisha na kuwarasimisha na kuwaongoza, hakuna mikakati inayowasimamia,” alisema Bi Fatma.

Alibainisha kuwa mpango wa kuboresha mashamba ya viungo, ambapo kuna vijana wanajihusisha na shughuli hizo: “Tutashirikiana na NMB kuwapa mafunzo na mikopo ili kuboresha bidhaa zao, tutawashika mkono ili kuhakikisha wanatoa huduma nzuri na bidhaa nzuri.

“Spice Tour haina viwango vinavyostahiki, pia wizara ina mkakati wa kuanza kuhusiha vijiji kuwe na Village Tourism ili kulinda utamaduni wetu. Hivi karibuni tulikwenda Pemba kukagua miradi yetu ili kuiendeleza zaidi na kuangalia namna gani vijana wanaweza kunufaika.”

Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa benki ya NMB, Bwana Filbert Mponzi alisema benki hiyo imekuwa ikifanya mambo mengi makubwa visiwani Zanzibar kwa lengo la kuinua sekta ya utalii, ndiyo maana wameamua kupeleka vituo vya mauzo 100 (Point of Sales) ambapo kwa sasa wanaiomba Wizara ya Utalii kuwaelekeza vituo watakaposambaza vifaa kwa ajili ya kufanyia malipo.

“NMB ndio benki kubwa zaidi nchini ambayo serikali ni mdau mkubwa, lakini pia inaongoza kwa kupata faida yaani kwa ukubwa, tunapoingia kwenye jukumu kama hili hatuna wasiwasi,” alisema Bwana Mponzi na kuongeza:

“Tumeshiriki katika mambo ya huduma kwa jamii mbali mbali hapa Zanzibar, tunatoa sana nchi nzima hakuna makubaliano tunayoingia bali tunasaidia kwa wenye uhitaji. Kama tumeamua kujifunga kwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar maana yake tutafanya kitu kikubwa katika utalii Zanzibar.”

Awali Bwana Mponzi alisema katika safari hii ya kuimarisha uchumi wa bluu na kwenda sambasamba na dunia kukuza uchumi kupitia mifumo ya kidigitali, NMB imekubaliana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale mambo kadhaa.

Ikiwemo kutoa elimu na kuhamasisha watu kuzidi kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo Zanzibar kupitia matamasha na promosheni mbali mbali.

Kuchagiza shughuli za kitalii Zanzibar kwa kuwekeza kwenye mfumo wa kidigitali zaidi utakaotumika katika makusanyo ya serikali katika vituo vyote vya utalii Zanzibar.

Kusambaza mashine za malipo yaani POS kwenye vituo vya makusanyo na vivutio vya utalii. Hii itawawezesha watalii kulipia ada na tozo zote kupitia kadi zao za Mastercard, Visa na UnionPay.

Lakini pia, kuongeza idadi ya POS katika maeneo ya hoteli, migahawa, sehemu za starehe na maduka ilikuruhusu malipo kupitia kadi. Hii itapunguza ulazima wa watalii kutembea na fedha taslim hivyo kuwawezesha kufanya malipo kwa njia salama na rahisi.

No comments:

Post a Comment

Pages