January 27, 2022

RC Malima aitaka Tarura kufuata utaratibu miradi ya barabara Tanga



Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima ameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mkoani hapa kuweka utaratibu wa kutoa taarifa kwa madiwani, wabunge na wananchi kuhusu mradi wanaotekeleza katika eneo husika.

Malima amesema hayo leo Jumatano Januari 26,  katika Kikao cha Bodi ya Barabara katika Mwaka wa Fedha 2021/22 cha kuangalia hali ya barabara mkoani Tanga.

Malima ambaye ni mwenyekiti wa hicho, amesema katika miradi mingi bila kushirikisha wananchi hasa pale wanapomwaga vifusi matokeo yake wananchi huona miradi hiyo kama kero kwao hususani wakati wa mvua.


"Zile hela ni za serikali si za mtu hivyo unatakiwa kumjulisha diwani, mbunge na mwananchi ambaye kimsingi ndiye mwenye mradi.

"Wakati mwingine unaweza kukuta vifusi vimemwagwa barabarani kama Km tano hivi vimekaa muda mrefu havifanyiwi kazi hadi mvua zinanyesha mwananchi anaona kero kwa sababu haelewi hakushirikishwa. Wote tunataka mambo mazuri katika Mkoa wa Tanga hivyo tushirikishane kufikia malengo," amesema.

Katika kikao hicho ambacho hufanyika mara mbili kwa mwaka, wajumbe ni Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala, wakuu wa wilaya, wabunge, wakurugenzi, madiwani, wenyeviti wa halmashauri, Kamati ya Usalama ya Mkoa na viongozi wanaohusika na barabara ikiwa Wakala wa Barabara (Tanroads) na Tarura, mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwamo hali za barabara mkoani hapa.

No comments:

Post a Comment

Pages