January 20, 2022

Serikali imepanga kupanda miti zaidi ya milioni 14 kupitia wanafunzi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Seleman Jafo akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na Vyuo nchini yenye kauli mbiu 'Soma na Miti'.

 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma
 
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Seleman Jafo amewaanigiza maafisa mazingira nchini kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kuhakikisha wanapanda miti milioni 14 ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia amewaagiza Maafisa Mazingira Nchini kuisimamia kampeni hiyo kwa kwenda mashuleni na vyuoni kuikagua miti hiyo ambayo itakuwa imepandwa.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo Januari 20,2022 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na Vyuo nchini yenye kauli mbiu 'Soma na Miti' amesema lengo ni  kila mwanafunzi wa shule ya msingi,sekondari na Chuo apande mti.

"Wizara ya elimu hili liangalieni kupitia Bodi ya mikopo maana ukame unazidi kuongezeka kila mwanafunzi amayechukua mkopo apande mti,”ameongeza.

Serikali imepanga kupanda miti zaidi ya milioni 14 kupitia wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo vikuu," amesema Waziri Jafo.
Waziri Jafo amesema wanafunzi waliopo katika shule za msingi na sekondari jumla wapo milioni 14.1 hivyo wamepanga kila mwanafunzi apande mti mmoja ili kufikisha idadi hiyo na kwa upande wa vyuo vya kati na vyuo vikuu kuna jumla ya wanafunzi 400,000 ambao nao wote watapanda miti.

Ameeleza kuwa ukosefu wa mvua katika siku za hivi karibuni unasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na kwamba  kuna haja ya kuhakikisha mazingira yanatunzwa ikiwa ni pamoja na miti kupandwa.

“Ukiangalia Nchi yetu ukame umeongezeka mvua ilikuwa inaanza kunyesha kuanzia mwezi wa tisa lakini  leo tuna Jnauari  mvua haijaanza hii ni kutokana na mabadiliko ya Tabia nchi kiwango cha maji katika mabonde na mito yetu yamepungua pia mgawo wa umeme umerudi kutokana na maji kupungua,”amesema.

Kwa upande wake,Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anaeshughulikia elimu,David Silinde ameagiza kufufuliwa kwa  Klabu za utunzaji  wa mazingira katika shule pamoja na Maafisa elimu kuisimamia kwa vitendo  kampeni ya soma na mti kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.

Awali,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Antony Mtaka aliwataka wale wenye viwanja vipya kupanda miti mitatu katika viwanja hivyo   ikiwemo wa kivuli na mti mmoja  a miwili ya matunda.

"Agenda ya utunzaji wa mazingira katika Mkoa  wa Dodoma ni  Kampeni endelevu," amesema Mataka.

Naye Meneja wa miradi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF),Tanzania Dk. Severin Kalonga amesema kuwa ofisi yao imekuwa ikifanya kazi zaidi ya miaka 25 hapa nchini hasa katika maeneo ya misitu, wanyamapori, vyanzo vya maji  kwamba wadau wao wakubwa ni serikali.

"Tunashukuru TAMISEMI, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),kwa kuandaa mpango mkakati wa kuondoa maeneo yaliyoharibiwa hapa nchini ili kuweza kutimiza lengo la kitaifa la kuboresha uoto wa asili," amesema Dk.Kalonga.

Ameongeza kuwa wameotesha miti mbalimbali hapa nchini kwa kushirikiana jiji pamoja na TFS na kwamba Kampeni hiyo inashabihiana na programu ambayo ipo ofisini kwao inayoitwa ' Wahifadhi wa misitu wa baadae'.

No comments:

Post a Comment

Pages