January 27, 2022

Serikali itaruhusu biashara ya punda na mazao yake watakapofikia milioni10


 


Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Hezron Nonga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.



Na Asha Mwakyonde,Dodoma

MKURUGENZI wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Hezron Nonga amesema serikali  haitatoa kibali  cha biashara ya punda na mazao yake  ikiwamo  uchinjaji kwa wawekezaji  hadi watakapofikia idadi ya milioni 10.

Haya aliyasema jijini Dodoma juzi katika mkutano wa kutathimini baada ya serikali kusitisha  Uchinjaji katika  kampuni za  Huacheng International Ltd ya mjini hapa na Fang Hua Investment Co.Ltd ya  mkoani Shinyanga alisema mkutano huo umekutanisha wataalamu kutoka Wizara ya Migugo na Uvuvi na wanaoshughulikia Ustawi wa wanyama katika nchi za Tanzania na Kenya.

Prof. Nonga alisema kuwa lengo mkutano huo  pia ni kubadilishana uzoefu na kuweza kupanga mipango ya pamoja kuendeleza mnyama punda.

Alisema kwa sasa wana punda ambao hawazidi 500,000 na kati yao labda  200 ni dume na 300 ni jike.

Alisema jike mmoja wa punda anabeba mimba miezi 13  na akizaa analea mtoto wake miaka mitano na kwamba punda mmoja  kwa miaka 10 anaweza akazaa mtoto mmoja  au asizae kabisa.

Prof. Nonga alifafanua kuwa wawekezaji wakati wanaanza kuchinja punda miaka ya 2016 hadi 2017  walikuwa wanachinja punda hao idadi yoyote pasipokuwa na ukomo.

"Walikuwa wanachinja idadi ya 400 kwa siku, idadi yavpunda waliopo ni Tanzania hawazidi  hata 700,000 kwa wakati ule  na waliendelea kuchinja  zaidi ya 400 kwa siku ikafika wakati punda hao wakaisha," alisema Pro.Nonga.

Alisema walikuwa na mkutano huo wa tathimini ambapo awali walikuwa wakifanya biashara ya kuchinja punda na  kuuza mazao yake tangu mwaka 2015 kwa wawekezaji wa kampuni hizo waliyokuja kuwekeza nchini.

Aliongeza kuwa mwaka 2021, Oktoba aliyekuwa Waziri wa Wizara  hiyo Mashimba Ndaki  alizuia Uchinjaji wa punda nchini baada ya wawekezaji kukiuka masharti.

"Leo tumekuja kukutana kwa ajili ya kufanya tathimini tangu zuio limefanyika  ni kitu gani kifanyike kama serikali ni nini kifanyike ili kuwe na mwendelezo mzuri wa ufugaji wa punda na kuweza kumtumia vema, "alisema.

Prof. Nonga alieleza kuwa baada ya kusitisha Uchinjaji  kukawa na wizi mkubwa wa punda kwenda nchi jirani na hiyo ikasababisha kupata  hasara na kwamba punda wengine walichinjwa ngozi zao kupelekwa nje ya nchi na Tanzania haikunufaka na chochote.

Mtafiti kutoka Taasisi ya  Utafiti wa Mifugo  Tanzania (TALIRI), Dk. Jonas Kizima alisema Kama mdau alishiriki katika utafiti kwa kushirikiana na taasisi tatu ikiwamo ASPA kuangalia ni namna gani punda hao wanafugwa katika jamii.

"Tulibaini biashara ya uchinjaji punda imeshamiri utafiti ulionesha aslimia 68 ya watu waliohojiwa  katika Wilaya tano za Iringa, Chemba, Monduli, Arusha walio wengi hawapendi uchinjaji wa punda," alisema.

Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2016 hadi 2019 baada ya kufanya tathimini walikuta punda waliochinjwa ni 88312.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Brooke East Africa kutoka nchini Kenya Dk. Raphael Kinoti  alisema kuwa hakuna nchi yoyote ya Afrika inayojua biashara punda.

"Biashara hii ni giza  kwa nchi za Afrika  nchi yoyote ambayo ilifanya biashara hii Viwanda vyote vimefungwa kila zao la punda ni biashara yenye pesa lakini wanaonufakika ni wawekezaji," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake  makuu mkoani Arusha  la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA), Livingston Masija alisema wanataka punda wafanye kazi katika sekta ya kilimo kuwezesha wananchi kujipatia tija.

" Tunataka punda waendelee kuwasaidia wananchi katika shughuli zao kila siku kama kuchota maji, kubeba matofali, kuni na mazao kutoka shambani kupeleka nyumabani," alisema.

Mdau na Mwenyekiti wa Kamati ya Shirikishi ya kuangalia suala la zima la biashara ya uchinjaji punda Profesa Dominic kambarage alisema  punda ndio mnyama pekee katika shughuli za binadamu.
 

No comments:

Post a Comment

Pages