Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Mhandisi James Kionaumela akikagua ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji Mkoko jimbo la Chalinze, pembeni ni Mhandisi wa Maji Yusufu Juma.
Mwenyekiti wa Kitongaji cha Mlingotini kijiji cha Mkoko, kata ya Mkata Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Husna Ramadhan akielezea furaha yake kuhusu mradi wa maji Mkoko.
Mhandisi wa Maji RUWASA Bagamoyo mkoani Pwani, Yusufu Juma akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoko, Mtoro Masimba kuhusu mradi wa maji kijijini hapo.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Mhandisi James Kionaumela akipanda ngazi kwa ajili ya kukagua ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji Mkoko jimbo la Chalinze.
Na Selemani Msuya, Chalinze
WANANCHI wa kijiji cha Mkoko, kata ya Msata jimbo la Chalinze, wilaya Bagamoyo mkoani Pwani, wamesema uamuzi wa Serikali kuwapelekea maji bombani utawaepusha kuuwawa na Mambo wa Mto Wami.
Mradi huo wa Maji Mkoko unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kupitia mkandarasi mzawa, ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Fedha hizo ni za mkopo usio na riba wa Sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambapo zitawezesha utekelezaji wa Sera ya Maji ambayo inayotaka kila mwananchi kuchota maji mita 400 kutoka nyumbani kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari wanaopita kuangalia utekelezaji wa miradi ya ustawi kijiji cha Mkoko Jimbo la Chalinze, Jumanne Mavula amesema ujio wa mradi huo kwake ni baraka na anaishukuru Serikali kuwafikiria na kuwapatia maji safi na salama.
“Mimi hapa nilipo nina mkono nusu, sababu ya hali hii niliyonayo ni Mamba wa Mto Wami ambaye alinikamata tukavutana akabakia na nusu ya mkono wangu,” amesema.
Mavula anasema umbali kutoka nyumbani kwake hadi mtoni ni kilomita moja, lakini hakukuwa na chanzo kingine cha kupata maji tofauti na Mto Wami ambapo kuna Mamba.
“Tangu mwaka 1991 nimekuwa na ulemavu huu kisa maji, kiuhalisia ufanisi wangu wa kazi umeshuka, lakini sina namna napambana hivyo hivyo, ila hili la maji kwa sasa tunaenda kukomboka. Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuona,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mlingotini Husna Ramadhani, amesema ujio wa maji hayo yatawaondolea changamoto ya kupata magonjwa na kuliwa na Mamba.
“Hapa kwetu watu zaidi ya 15 wameshaliwa na Mamba, ila sasa tumekomboka, pia maji machafu tutakuwa hatunywi tena. Rais Samia ameupiga mwingi. Mungu amuongezea siku za kuishi ili afanye mengi,” amesema
Naye Asha Chavula amesema baada ya kupata maji safi na salama anatarajia kujikita na shughuli nyingine za uzalishaji, hivyo kuchochea maendeleo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkoko Mtoro Masimba, amesema wamepokea mradi huo kwa mikono miwili na kuahidi kushirikiana na wanakijiji kulinda na kuutunza.
Amesema kijiji hicho ambacho kina wananchi zaidi ya 1,500 kimepitia wakati mgumu wa kukosa maji safi na salama, hivyo walichofanya RUWASA ni cha kupongezwa.
“Miaka 50 hatuna maji safi na usalama, lakini pia tumepoteza zaidi ya watu 30 na zaidi ya 50 kujeruhiwa na Mamba, hivyo tunadiriki kusema tumekombolewa na Rais Samia,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mkoko B, Jumanne Mdihile amesema kinachofanywa na RUWASA ni utekelezaji wa Ilani ya chama, hali ambayo itawasaidia kujibu hoja za wapiga kura kuhusu maji.
“Mradi huu umetoa majibu ya maswali ya wapiga kura wetu ambao tuliwaahidi kuleta maji. Rais Samia ametukomboa,” amesema.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo, Mhandisi James Kionaumela amesema Mradi wa Maji Mkoko umeenda kumuendeleza mwananchi wa kijiji hicho/
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa Sh.milioni 348 ambapo fedha hizo zinatumika kusambaza mabomba kilomita 16.2, ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji na tenki la lita 50,000.
“Mradi huu utanufaosha wananchi 1,742, ambao wamekuwa wakipitia wakati mgumu wa kupambana na Mamba wakati wakitafuta maji,” amesema.
Mhandisi Kionaumela amesema ujenzi wa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 80 ambapo wamefikisha huduma za maji kwenye taasisi za elimu, dini na nyinginezo.
Meneja huyo amesema upatikanaji wa maji Chalinze vijijini kwa sasa ni asilimia 69 na mijini ni 79 na matarajio yao ni ifikapo 2025 kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inavyowata kufikia asilimia 85 ya maji vijijini na 95 mijini watafikia.
No comments:
Post a Comment