April 22, 2022

Mbarawa aitaka TMA kuongeza mapato kisheria

Na Irene Mark

BARAZA la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa limeagizwa kuongeza wigo wa mapato na kutoa elimu ya uchangiaji wa gharama za matumizi ya taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Agizo hilo limetolewa leo Aprili 21, 2022 na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza hilo la wafanyakazi ambalo pamoja na mambo mengine limejadili bajeti ya TMA kwa mwaka 2022/2023.

 

Profesa Mbarawa amewapongeza wadau wote wanaoonesha ushirikiano hasa waliojitokeza kusajili vituo vyao na kutoa tozo za uchangiaji wa gharama za utoaji wa huduma mahususi kwa sekta ili kukidhi matakwa ya sheria.
 
“Nimefurahi kusikia kuwa mpo katika majadiliano ya kukubaliana tozo mpya kwa sekta nyingine, mmetoa mfano wa sekta ya ujenzi, hata hivyo kuna jambo ni vizuri mkalifamu na kulifanyia kazi, majadiliano yenu yajikite kuwaelimisha wadau kuitekeleza Sheria namba 2 ya mwaka 2019 inayoisimamia mamlaka yenu.

“...Kuchangia huduma ni suala la kisheria hivyo kila mdau hana budi kulitekeleza. Hakikisheni mnakusanya mapato kwenye maeneo yote yaliyoainishwa na sheria kwamba yanazitumia huduma za hali ya hewa kibiashara. Wizara yangu iko tayari kuwasaidia endapo kutatokea changamoto yoyote katika utekelezaji wa jukumu hili la ukusanyaji wa mapato,” amesema Profesa Mbarawa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa TMA, Dk. Agnes Kijazi amesema baraza hilo lenye wajumbe 98 kutoka vituo mbalimbali vya mamlaka hiyo, limeanzishwa kwa mujibu wa mkataba wa Baraza kati ya Menejimenti na TUGHE.


“Kikao hiki cha baraza ni mwendelezo wa utekelezaji wa mkataba uliopo unaotarajiwa kuisha mwaka huu 2022.

“Wafanyakazi wa TMA wameendelea kufanyakazi kwa bidii ili kuhakikisha jukumu tulilokabidhiwa na serikali la kutoa, kuratibu na kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini, linatekelezwa kwa ufanisi,” amesema Dk. Kijazi.
 
Amesema kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchangiaji gharama za utoaji wa huduma za hali ya hewa zinazotumika kibiashara, TMA imepewa nguvu ya kukusanya mapato kutoka katika sekta mbalimbali ikiwemo usafiri wa anga, maji, mafuta na gesi, viwanda, utalii, ujenzi, madini, usafiri wa aridhini, mazingira na nishati.

Dk. Kijazi amesema kwa sasa mamlaka hiyi imeanza kukusanya mapato kutoka sekta ya usafiri wa anga wakati usafiri wa maji na sekta ya madini unakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa watumiaji wa huduma za hali ya hewa kuhusu kanuni ya kuchangia huduma.

“Wengi wanapenda kuzitumia huduma kibiashara lakini hawapendi kuchangia.  Hata hivyo Mamlaka inaendelea kutoa elimu ili watekeleze takwa hilo la kisheria,” amesisitiza mkurugenzi huyo.


No comments:

Post a Comment

Pages