SERIKALI
imesema katika kuhakikisha adha ya kukatika umeme inaisha inatarajia
kuzalisha megawati 200 zinazotokana na chanzo Cha Jotoardhi kabla ya
mwaka 2025.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba, wakati wa ziara yake ya kukagua vyanzo vya nishati ya Jotoardhi
vya Kiejo-Mbaka na Ngozi mkoani Mbeya.
Amesema
Tanzania kuna jumla ya maeneo 52 yanayoweza kutoa nishati ya Jotoardhi
ambayo tayari yameshatambuliwa, hivyo watayatumia kutimiza lengo Hilo la
kuzalisha Megawati 200 ifikapo 2025.
Ameeleza
kuwa, kwa ujumla, Serikali ina mpango wa kuongeza megawati 1,100
zinazotokana na Nishati Jadidifu kabla ya mwaka 2025 na hizo megawati
zitatokana na vyanzo mbalimbali kama vile Jotoardhi, Jua na Upepo.
Ameongeza
kuwa, Wizara ya Nishati inaweka nguvu kubwa katika kuendeleza vyanzo
vya nishati ya Jotoardhi kwa sababu vyanzo hivyo haviishi na hivyo
ukaguzi alioufanya katika maeneo hayo ya Jaothemo utasaidia Serikali
kuona hatua stahiki za kuchukua ili kuendeleza vyanzo hivyo.
“Kipindi
cha ukame maji yanaweza kupungua, lakini Jotoardhi katika kipindi cha
ukame au mvua, mvuke unaotoka chini ya ardhi uko palepale," amesema
Katibu Mkuu Mramba.
Amesema
kuwa, nchi ya Kenya ina zaidi ya megawati 1,100 zinazotokana na
Jotoardhi na Tanzania kutokana na eneo lake kubwa kupitiwa na Bonde la
Ufa kuna uwezekano wa kupata umeme mwingi zaidi unaotokana na nishati
hiyo.
“Mfano hapa mkoani
Mbeya katika eneo hili la Rungwe kumeonekana kuna uwezekano mkubwa wa
kutoa nishati ya Jotoardhi kwa sababu tawi moja la Bonde la Ufa
limeingia katika eneo hili na Tawi jingine limeelekea upande wa Malawi,"
ameeleza Mhandisi Mramba
Kwa
upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi
Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba amesema kuwa, eneo la
Kiejo-Mbaka linaweza kuzalisha megawati 60 zinazotokana na Jotoardhi.
Amesema
kuwa, Serikali imetoa takribani Sh.bilioni 20 kwa ajili ya uendelezaji
wa eneo hilo na sasa wamenunua mtambo wa kuchoronga eneo hilo, na
kwamba, wataalam wa TGDC na wahisani wameshirikiana katika kufanya
tafiti zote zinazotakiwa.
Ameongeza
kuwa katika eneo la Ngozi, inategemewa kuwa litazalisha megawati 70
zinazotokana na Jotoardhi na kwamba TGDC imejipanga vizuri katika
kuhakikisha kuwa Tanzania inapata umeme kutoka kwenye nishati hiyo
Jadidifu.
No comments:
Post a Comment