April 27, 2022

Taasisi za mazingira Afrika Mashariki zazindua azimio la pamoja kupinga matumizi ya plastiki zitumikazo maramoja

 Zoezi la ukusanyaji taka likifanywa na vijana mabalozi kutoka taasisi ya Nipe Fagio kabla ya taka hizo kuchambuliwa na kutenganishwa kulingana na aina za chapa. Zoezi lilifanyika katika fukwe za Kawe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. 

 

 

Dar es Salaam: Tanzania - Taasisi ya Nipe Fagio ikishirikiana na taasisi nyingine za Afrika Mashariki za Cejad (Kenya), Bio Vision Africa (Uganda), na GER Global (Rwanda) pamoja zazindua azimio lenye lengo la kukusanya saini zaidi ya 15,000 kupinga matumizi ya plastiki zitumikazo maramoja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha imelenga kuhimiza utekelezwaji wa sheria utazuia wazalishaji wa plastiki zitumikazo mara moja kuendelea na uzalishaji wao unaopelekea uchafuzi wa mazingira.

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki katika maadhimisho ya Siku ya Dunia (Earth Day) Aprili 22 yaliyofanyika katika ufukwe wa Kawe, Bi Rocha alisema plastiki zitumikazo maramoja zinaendelea kusababisha huaribifu wa mazingira katika jumuiya yote ya Afrika Mashariki.

 

Uzalishaji usiosimamiwa wa plastiki zitumikazo maramoja kwa ajili ya vifungashio unachangia kuleta madhara ya kiafya, mafuriko, mabadiriko ya tabia nchi, na upatikanaji mkubwa wa plastiki katika mito yetu na bahari.

 

Alisema kuwa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki Tanzania, Kenya, Uganda, na Rwanda kwapamoja wameandaa mapendekezo yatakayopelekea utengenezaji wa sheria moja itakayotoa muongozo wa jinsi gani ya kupambana na uchafuzi wa mazigira utokanao na plastiki.

 

Ili kufanikisha lengo hilo, alisema kuwa watawasilisha mapendekezo ya sheria katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha kwa ajili kuleta msukumo zaidi katika mabunge ya ukanda huo.

 

“Tukiwa katika zoezi la kutambua nani anaongoza katika uchafuzi wa mazingira utokanao na vifungashio vya plastiki katika mazingira yetu, tunaliweka mbele tatizo la uchafuzi utokanao na plastiki zitumikazo mara moja na uhitaji wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuchukua hatua haraka kutatua tatizo kwa kuangalia mnyororo mzima wa uzalishaji wa plastiki,” alisema Ana.

 

Ili kuweka msisitizo kwenye hatua hiyo, Nipe Fagio na taasisi nyingine wadau wa mazingira Arika Mashariki wataweka msukumo kwenye kusaini azimio la pamoja ikiwa dhumuni la kutilia mkazo lengo lao.

 

Alisema kuwa taasisi hizo zinahasa kuwepo kwa katazo la matumizi ya plastiki zitumikazo maramoja na kushawishi nchi za Afrika Mashariki kutunga na kufanyia kazi sheria ambazo zitaunga mkono uzalishaji endelevu na utumiaji wa bidhaa za plastiki (Kama vile Uwajibikaji wa Mzalishaji) pamoja na sheria zitakazo kuza utendaji bora na endelevu wa utunzaji taka kama vile mifumo ya taka sifuri, utumiaji tena, na urejelezaji wa baadhi ya makundi ya taka za plastiki.

 

Taasisi hizo pia zinataka utekelezwaji wa makubaliano ya kimataifa yanayolenga kulinda mazingira, pamoja na kushawishi serikali kusaini makubaliano/mikataba ya kimataifa inayolinda mazingira kwa ujumla. 


Kusaini azimio hilo tembelea https://bit.ly/SUPfreeEAC_Petition 

 


Zoezi la uchambuaji na utenganishaji wa taka kulingana na aina za chapa likifanywa na vijana mabalozi kutoka taasisi ya Nipe Fagio. Zoezi lilifanyika katika fukwe za Kawe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

No comments:

Post a Comment

Pages