Na Benny Mwaipaja, Washington DC
Nchi
za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimewasilisha
maombi ya kupatiwa mkopo wenye masharti nafuu kwenye Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB), kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka
Uvinza-Msongati- Gitega, yenye urefu wa Km 939, uliokisiwa kugharimu
dola za Marekani milioni 900.
Majadiliano
ya awali kati ya Benki hiyo na Mawaziri wa Fedha wa Nchi hizo tatu,
Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba wa Tanzania, Mhe. Nicolous Kazadi wa
DRC na Mhe. Dkt. Domitien Ndihokubwayo wa Burundi, yamefanyika
Washington DC, kando ya Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika
la Fedha la Kimataifa-IMF, Washington DC, nchini Marekani.
Akizungumza
baada ya kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa reli hiyo ni muhimu kwa ustawi na
maendeleo ya kiuchumi ya nchi zote tatu kwa sababu itakapokamilika
itarahisha usafirishaji wa mizigo, abiria na kukuza biashara na
maendeleo ya viwanda ya nchi hizo.
Alisema
kuwa mradi huo ni mkubwa ndiyo maana nchi hizo zimekubaliana kutafuta
mikopo nafuu kutoka vyanzo mbalimbali na pia kwa kutumia fedha
zitakazotengwa kwenye bajeti zao za ndani ili mradi huo uanze kujengwa.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Nnenna Nwabufo, alisema kuwa Benki yake
inatambua umuhimu wa mradi huo kiuchumi, kisiasa na kijamii na kwamba
utasaidia pia kuziunganisha nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki
na ni muhimu kwa ajili ya utengamano wa nchi hizo.
Aliahidi
kuwa Benki yake itashiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa mradi huo
unajengwa kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo pamoja na maendeleo ya
kiuchumi ya nchi zinazoshiriki katika kujenga mradi huo muhimu.
No comments:
Post a Comment