Kikao kikiendelea.
Faraja Mpina na Chedaiwe Msuya -WHMTH
NAIBU Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla ametoa
siku nane kuanzia Aprili 27 /2022 hadi Mei 5/2022 kwa watendaji wa Mkoa
wa Singida kusimika nguzo zenye majina ya barabara na mitaa pamoja na namba za
nyumba katika halmashauri zote saba za mkoa huo.
Akizungumza katika ziara
yake mkoani hapo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya
Anwani za Makazi, Naibu Katibu Mkuu amesema eneo pekee ambalo mkoa huo umefanya
vizuri ni ukusanyaji wa taarifa za wakazi na makazi, na maeneo mawili
yaliyosababisha wawe katika nafasi za mkiani ni kutokuweka nguzo zenye majina
ya barabara na mitaa pamoja nan amba za nyumba,
“Nikiangalia muda
uliobaki na nilichokisikia hapa haviendi sawa, wakurugenzi na watendaji wa
halmashauri hakikisheni ifikapo Mei 5 nguzo zenye majina
ya barabara na mitaa zisimikwe na namba za nyumba ziwekwe, kuanzia Mei 6 timu ya wataalamu ya Wizara itakuja kufanya uhakiki “physical
verification” ya uwekaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi katika mkoa huu”, alisema Abdulla.
Ameongeza kuwa, zoezi la
uwekaji wa Anwani za Makazi lisipokamilika kwa muda uliopangwa litakwamisha
zoezi la sensa ya watu na makazi, na akiangalia mwenendo wa uwekaji wa nguzo
zenye majina ya barabara na mitaa na uwekaji wa namba za nyumba kwa halmashauri
zote za mkoa wa Singida utekelezaji wake ni wastani wa asilimia 3 hadi 4.
“Ni aibu hata sie watekelezaji
wa operesheni hii bado hatuna Anwani za Makazi, mpaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Singida hauna kibao cha Anwani ya Ofisi, tuhakikishe ndani ya siku mbili hadi
tatu kuanzia leo tarehe 27, Mei, 2022 ofisi zote za Serikali ndani ya Mkoa wa
Singida zimewekwa Anwani za Makazi, na taarifa ya utekelezaji iwasilishwe
Wizarani kupitia Meneja wa Mkoa wa Singida wa Shirika la Posta Tanzania”. alisisitiza.
Awali, taarifa za
utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi katika Mkoa wa Singida ziliainisha
changamoto za utekelezaji zilizojitokeza
ikiwemo uhaba wa fedha ambapo Naibu Katibu Mkuu aliipangua hoja hiyo kwa
kuwakumbusha kuwa Mamlaka ya juu inapotoa agizo hakuna visingizio kwenye
utekelezaji.
“Muongozo upo, bajeti ni
ndogo lakini ni lazima zoezi hili likamilike, ukishakusanya taarifa kwenye kuandika
namba za nyumba tafuteni rangi, chaki au mkaa ili mradi namba ikiandikwa
ionekane ili watu wa sensa wakija wajue hii ni nyumba namba fulani, iliyopo
mtaa fulani na mwananchi atakayetaka kuweka namba yake kulingana na muongozo
aruhusiwe.”
Viongozi na watendaji wa
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wameendelea na ziara ya
kukagua utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi hasa katika mikoa ambayo
haifanyi vizuri.
Mikoa takribani 20 imefikiwa kwa ukaguzi na uhamasishaji wa utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi . |
No comments:
Post a Comment