May 28, 2022

BRELA yakusudia kufuta makampuni 5,676

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekusudia kufuta makampuni 5,676 ambapo kati ya hayo makampuni 5,284 ni yaliyosajiliwa hapa nchini na makampuni 392 ni ya yaliyosajiliwa nje ya nchi na kupata hati ya Utambuzi.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa katika  Ukumbi wa Mikutano kwenye Ofisi za taasisi hiyo Jijini humo.

Amesema kuwa wamekusudia kufuta makampuni hayo kwa kushindwa kukidhi takwa la kisheria la kuwasilisha taarifa za mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa hapa nchini au mizani ya mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 15.

“Endapo kampuni husika, wanahisa au wadeni wa kampuni ikiwemo taasisi za kifwdha na watumishi wa kampuni wanaamini kwamba kampuni iliyoko kwenye orodha hii inafanya biashara na kwamba inapaswa kubaki kwenye Daftari la Makampuni watoe taarifa kwa Msajili wa Makampuni”. Amesema

Aidha BRELA imetoa rai kwa makampuni yaliyosajiliwa chini ya sheria ya Makampuni, sura 212 ambayo hayakuorodheshwa kwenye Orodha ya awamu ya kwanza, kutekeleza matakwa ya sheria hiyo kwa kuwasilisha taarifa za mwaka ili kuepuka kufutwa kwenye Daftari la Makampuni kwani zoezi hili ni endelevu.

Amezitaja  sababu nyingine zinazofanya kampuni kuonekana hazifanyi biashara ni pamoja na, kukosa mtaji wa biashara, kuelemewa na migogoro baina ya wamiliki, kushindwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa na hivyo kutokuwa na sababu ya kuendelea na uendeshaji wakampuni na kutokuwa na uelewa kuhusu wajibu wa Wakurugenzi na Wamiliki wa Kampuni.

 

No comments:

Post a Comment

Pages