May 31, 2022

Issa Nambole Mwenyekiti mpya CCM Kisutu


Issa Nambole (kushoto) mshindi wa nafasi ya Uenyekiti wa CCM tawi la Kisutu Ilala Dar es Salaam akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa tawi hilo, Komme Ridhiwani, muda mfupi kabla ya kupiga kura.
Na Mwandishi Wetu

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala Athumani Chillah, amemtangaza Issa Nambole kuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Kisutu, Dar es Salaam.

Akisoma matokeo ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa CCM Tawi la Kisutu, Chillah alisema Nambole ameshinda kwa kura 62 dhidi ya kura 36 alizopata mshindani wake, Komme Ridhiwan aliyekuwa akitetea nafasi yake.

Uchaguzi huo wa marudio umefanyika leo Mei 30,2022 kwenye ukumbi wa Shule ya Msingi Kisutu jijini hapa ukisimamiwa na viongozi wa CCM Wilaya Ilala akiwemo Saidi Almasi ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wilayani humo.

“Kwa mamlaka niliyopewa na chama changu CCM kutoka Wilaya ya Ilala, napenda kutangaza matokeo ya uchaguzo huu uliokuwa na wapiga kura 107.

“Kati yao waliopiga kura ni 98; hakuna kura iliyoharibika bwana Nambole ameshinda kwa kura 62 wakati mgombea mwenzie bwana Ridhiwani amepata kura 36 hivyo basi mshindi wetu ni Nangole amekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Kisutu kuanzia sasa,” alisisitiza Chillah.

Baada ya matokeo hayo, Ridhiwani alikubali matokeo na kuwashukuru wapiga kura wote huku akiahidi kumpa ushirikiano mwenyekiti mpya.

“Issa ni kaka yangu amenipokea kwenye chama tuna mahusiano mazuri sana nakubali ameshinda kwa kishindo... mimi mdogo wako nipo tayari kukusaidia katika kukijenga chama.

“Hii ndio maana ya uchaguzi kuna kushinda na kushindwa asanteni wote mlioshiriki kutupigia kura,” alisema Ridhiwani.

Akiwashukuru wapiga kura wote, Mwenyekiti Nambole alisema makundi ya wakati wa kampeni yameisha sasa wote waungane kukiimarisha chama chao.

“Nawashukuru sana kwa kuniamini maana uchaguzi ni uchaguzi tu presha na makundi yalikuwepo, ila baada ya matokeo haya nayo yamekwisha... namshukuru Mungu umeisha salama na sasa ni muda wa kukijenga chama ili kwenda kushika dola mwaka 2025 kwa ngazi zote.

“Tumemaliza uchaguzi huu sasa tuelekeze nguvu kwenye chaguzi za juu ili 2025 tuhakikishe tunashika dola na hii ni kwa umoja sio kazi ya viongozi pekee, kidumu Chama Cha Mapinduzi,” alihitimisha Nambole.

No comments:

Post a Comment

Pages