May 12, 2022

Jeshi la Polisi Kanda Maalum lawashikilia 23 kwa wizi wa kutumia silaha



 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu 23 kwa tuhuma matukio ya uhalifu wa wizi na unyang'anyi wa kutumia silaha ikiwemo visu na mapanga.

Akizungumza na wanahabari jijini humo Kamanda wa kanda hiyo Jumanne Muliro amesema watu hao wamekamatwa katika mwendelezo wa oparesheni kali ya mtaa kwa mtaa pamoja na kata kwa kata inayolenga kudhibiti matukio ya uhalifu.

" Wahalifu wanadaiwa kupanga njama za kufanya uhalifu kufikia jana Mei 12 tumewakamata wengine 23 wanaotumia silaha kufanya wizi wa kutumia silaha," amesema Kamanda Muliro.

Amebainisha kuwa watuhumiwa 11 waliofanya tukio uhalifu eneo la Kitunda Machi 27 mwaka huu walikamatwa na kwamba walifanikiwa kupora runinga 3 huku akisisitiza kupitia intelejensia walitiwa nguvuni.

Kamanda Muliro ameonya watu kuacha tabia ya kuzusha matukio ya uhalifu wanapoona vikundi vya vijana wakiwa wanne wamekaa kwa kutoa taarifa ambazo si za ukweli kwani zinazua taharuki na hofu kwa wananchi.

Amefafanua kuwa vikosi vya jeshi la polisi vinaendelea kupambana na uhalifu jijini huku akiwaonya wazazi wanaofaidika na matunda ya wizi ya watoto wao watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.


No comments:

Post a Comment

Pages