May 14, 2022

MADIWANI IKUNGI WATAKIWA AJENDA YAO KUBWA IWE NI KUKUSANYA MAPATO

Zawadi kwa washindi wengine wa ukusanyaji mapato zikitolewa. Anayepongezwa kushoto ni Afisa Mtendaji Kata ya Muhintiri, Bahati Mkungile.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Ally Mwanga (katikati) akiongoza kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya tatu kilichoketi wilayani humo juzi na jana.Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Diwani wa Kata ya Mkiwa Stephen Mtyana na kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Justice Kijazi.




Na Dotto Mwaibale, Ikungi


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametakiwa ajenda yao kubwa kuwa ni ukusanyaji wa mapato ili wilaya hiyo iweze kupaa kiuchumi.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ally Mwanga wakati akiongoza kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya tatu kilichoketi wilayani humo jana na leo.
Mwanga alisema halmashauri yoyote haiwezi kupiga hatua ya maendeleo bila ya kuwa na mapato ya kutosha hivyo madiwani wanakila sababu ya kuwa mstari wa mbele katika kukusanya mapato kwenye maeneo yao.

" Ninyi madiwani ndio tunaowategemea kwa kiasi kikubwa kuhamasisha ukusanyaji wa mapato kwenye kata zenu kwani huko ndiko chimbuko la mapato hivyo ni jukumu lenu kuongeza bidii ya ukusanyaji kwa kushirikiana na watendaji wenu wa kata" alisema Mwanga.

Alisema hivi sasa ajenda yao kubwa iwe ni kukusanya mapato tena kwa nguvu zao zote ili halmashauri hiyo iwe kinara kwa kukusanya mapato hapa nchini.

Katika hatua nyingine Mwanga alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Justice Kijazi kuifumua idara ya afya kutokana na kuwa na changamoto nyingi za kiutendaji kutokana na baadhi ya watumishi wa idara hiyo kufanya kazi kwa mazoea hivyo kukwamisha mambo mengi.

"Mkurugenzi nakuagiza ifumue idara ya afya kwa kuwabadilisha vituo watendaji wake, waliopo hapa wilayani wapeleke huko vijijini na wale wenye uwezo waliopo vijijini walete hapa wilayani itasaidia kurudisha uwajibikaji na kupunguza haya malalamiko ya kila siku ambayo yanaichelewesha kimaendeleo halmashauri yetu" alisema Mwanga.

Hata hivyo Kijazi alieleza kwamba changamoto hiyo itamalizika hivi karibuni kwani wanategemea kumpata mganga mkuu wa wilaya baada ya wa awali kuhama na nafasi hiyo kushirikliwa na kaimu.
"Maagizo yako nimeyapokea  lakini tunategemea kumpata mganga mkuu wetu hivi karibuni naamini changamoto hii itakwisha mara baada ya kufika" alisema Kijazi.

Akizungumzia ukusanji wa mapato Kijazi alisema itakuwa haina maana ya kukusanya mapato mengi na matumizi yake yakawa makubwa ambapo alitoa wito kwa watendaji kuzingatia jambo hilo ili kuyalinda mapato hayo.

Alisema mapato ndio injini ya halmashauri hivyo ni jukumu la kila mmoja wao kuhakikisha yanakusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali kwani ndiyo yanayosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika baraza hilo madiwani walipata fursa ya kutoa taarifa mbalimbali ya matumizi ya fedha katika miradi na kujadiliana mbinu za ukusanyaji wa mapato huku kata vinara kwa ukusanyaji mapato zikipongezwa huku zile ambazo zilionekana kushuka kimapato zikitakiwa kuongeza bidii  kwa kujifunza kutoka kwa zile zilizofanya vizuri.

Aidha watendaji wawili wa kata mbili zilizoongoza kwa ukusanyaji wa mapato walizawadiwa pikipiki kila mmoja huku wengine wakipatiwa fedha taslimu ikiwa ni motisha na kuwapa ari ya kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.

Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Kizigo akizunguza wakati akitoa salamu za Serikali aliwaomba waratibu wa zoezi la Sensa ya watu na makazi kuwahimiza watendaji wa vijiji na vitongoji kutangaza nafasi za kuomba  ajira ya muda ya  ukalani na usimamizi wa zoezi  hilo huku akiwaomba watoe kipaumbele  kwa vijana wenye sifa wa wilaya hiyo kabla ya kuwachukua wale wanaotoka nje ya wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages