May 28, 2022

Mwenge wapima mamia VVU Tanga


Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa akitoa taarifa ya shughuli zilizofanywa na mwenge wa uhuru wilayani Tanga.



Na Mwandishi Wetu, Tanga


WATU 577 wamepimwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika mkesha wa Mwenge wa Uhuru uliowasili mkoani Tanga jana ukitokea Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Ukiwa mkoani hapa, mwenge umekagua na kuzindua miradi saba ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanga Mjini yenye thamani ya Sh. bilioni 20.037.

Akitoa takwimu za upimaji wa VVU, Uviko-19 na malaria katika mkesha huo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa amesema katika watu 577 waliopima VVU wanawake walikuwa 372
na wanaume 202 huku waliokutwa na maambukizi wakiwa watatu sawa na asilimia 0.51.

"Aidha, kuna waliopimwa maralia hawa walikuwa 161 na waliokutwa na maambukizi ni wanne na waliochanja chanjo ya Uviko-19 walikuwa 443 lakini pia tulikuwa na shughuli ya uchangiaji wa damu ambapo  watu tisa walichangia," amesema DC Mgandilwa.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Sahili Geraruma amewataka wananchi mkoani Tanga kuzingatia ujumbe wa mwenge kuhusu Sensa ya Watu na Makazi.

"Mwenge pia unawakumbusha kuzingatia afya njema kwa kupata lishe bora, mapambano dhidi ya malaria, dawa za kulevya na kupiga vita rushwa," amesema.

Mwenge wa Uhuru leo utakuwa katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment

Pages