RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussen Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa wiki ya ubunifu na mashindano ya kitaifa ya sayansi, Teknolojia na ubunifu (MAKISATU) itakayoanza Mei 15 hadi Mei 20,2022 Jijini Dodoma.
Hayo
yameelezwa Jijini hapa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kuanza kwa
maadhimisho hayo na kueleza kuwa mashindano
hayo yataibua, kutambua, kuadhimisha, kujenga, kukuza na kuendeleza
ubunifu wa Watanzania katika nyanja za Sayansi na Teknolojia ili
kuchangia juhudi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Alisema
Rais Mwinyi atasindua rasmi maadhimisho hayo Mei 16 huku Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philp Mpango akitarajiwa
kufungua maonesho hayo Mei 19 mwaka huu.
Alifafanua
kuwa maadhimisho ya wiki ya MAKISATU ni sehemu ya mikakati ya Serikali
ya awamu ya sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi na kwamba
maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi ya mikoa na Taifa .
"Katika
ngazi ya mikoa maadhimisho hayo yanaratibiwa kwa ushirikiano kati ya
wizara ya hii,COSTECH na programu ya FUNGUO chini ya Shirika la UNDP
kupitia kumbi za ubunifu,vituo vya ubunifu,taasisi za umma na binafsi
Katika mikoa husika ambapo uratibu huu inahusisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI
kupitia maafisa maendeleo ya jamii,"alisema
Alisema
Katika ngazi zote mbili,mikoa na Taifa, MAKISATU yataambatana na
matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilele chake yatakayolenga kupata
washindi Kwa mwaka 2022 Katika ngazi ya kitaifa,majukwaa ya majadiliano
kuhusu maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu nchini yanayohusisha
utafiti na ubunifu.
"Mashindano
haya pia yatahusisha Serikali na wadau mbalimbali wa ubunifu na
maendeleo ndani na nje ya nchi Kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja
katika kuhamasisha maendeleo na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya
uchumi na jamii,"alisema
Alibainisha kuwa katika maadhimisho hayo pia kutakuwa na mafunzo na semina kwa wabunifu ikiwemo elimu na ujasiriamali.
Kutokana na hayo Waziri huyo mwenye dhamana ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
alitumia
nafasi hiyo kuwataka wabunifu na wananchi wote kushiriki katika
maadhimisho hayo na kuendelea kutumia bunifu mbalimbali zinazotokana na
watanzania katika shughuli za maendeleo.
Wiki hiyo pamoja na mambo mengine Kwa mwaka huu imebeba kaulimbiu ya "Ubunifu kwa maendeleo endelevu".
No comments:
Post a Comment