May 30, 2022

Wanafunzi 987 wapata elimu ya hedhi salama

 

Mwanamitindo Flaviana Matata ambaye ni Mkurugenzi wa Flaviana Matata Foundation (kushoto) na Meneja Mahusiano wa MST, Esther Shedafa, wakigawa taulo za kike na zawadi nyingine kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukandwe wilayani Magu, Mwanza juzi. (NA MPIGA PICHA WETU

 

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
 
SHIRIKA la Marie Stopes Tanzania (MST) kwa kushirikiana na Flaviana Matata Foundation, wameadhimisha siku ya hedhi salama kwa kutoa elimu kwa wanafunzi 987 wa kike na kiume wa Shule ya Sekondari ya Bukandwe, wilayani Magu Mkoa wa Mwaza.

Siku ya hedhi duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 28 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu maswala ya hedhi kwa msichana na kuhamaisha upatikanaji na matumizi ya maji safi na taulo za kike hasa walio katika mazingira magumu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Meneja Mawasiliano wa MST, Esther Shedafa imeeleza kwamba dhumuni la maadhimisho ya siku ya hedhi ni kumtaka binti ajisitiri vizuri akiwa kwenye siku zake huku akiendelea na masomo yake na shughuli nyingine.

Shedafa amesema wanafunzi wakiume wameshiriki kwenye siku hiyo ili kuondoa unyanyapaa pale msichana anapokuwa kwenye hedhi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo siku ya hedhi mwaka huu imebebwa na kauli mbiu isemayo ‘Hedhi iwe kama ni moja ya Maisha ya kawaida kwa msichana na mwanamke’.

“Hii kaulimbiu ina maana kwamba tuwe na Dunia ambayo hakuna mtu ataachwa nyuma au atashindwa kufikia malengo yake au kufanya shughuli zake za kila siku kwa sababu tu anaingia kwenye siku za hedhi,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo kutoka kwa Shedafa.
 
Hata hivyo MST na Flaviana Matata Foundation wametoa wito kwa mashirika binafsi, walimu na serikali kusisitiza utolewaji wa elimu ya hedhi kwa vijana wa kiume na wa kike ili kuwasaidia wasichana kutambua mabadiliko ya mwili  na kukabiliana nayo ikiwemo namna bora ya kujisitiri na kuondoa unyanyapaa  pale msichana anapokuwa kwenye hedhi .

“Hedhi ni kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa, wakati ambao kwa kawaida unarudi kila mwezi ambapo hutokwa na damu kwenye uke kwa sababu kijiyai kilichokomaa na kutoka nje ya kifuko cha vijiyai kisipopata mbegu ya mwanamume baada ya siku moja kinaharibika harakaharaka.

“...Na hapo ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi, iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inajiengua  na kutoa damu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Shedafa.

Ilieleza kwamba hedhi salama ni ile ambayo inahusisha mtoto wa kike kupata mahitaji yake yote muhimu akiwa kwenye siku zake za hedhi ambayo ni taulo za kike maji safi na salama na sehemu ya kubadilishia.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa mtoto wa kike akipata hedhi salama basi ataondokana na matatizo ya kiafya ikiwemo miwasho, fangasi, maumivu na hedhi bila kutokwa damu nyingi, hivyo huwa hedhi yenye amani na furaha.

“Suala la hedhi halipaswi kuwa kero kwa mtoto wa kike. Hata hivyo, imekuwa tofauti kwa watoto wengi wa kike ambao hupata wasiwasi na kukosa raha pindi wanapokaribia mzunguko wao.”


MST imewataka wananchi kuwasiliana nao kwa namba ya simu 0800753333 bila malipo katika vituo vyao
vilivyopo Dar es salaam, Zanzibar, Mwanza, Musoma, Kahama, Arusha , Iringa , Makambako na Kimara.
 
Hata hivyo baada ya mafunzo mashirika hayo yaliwashika mkono wanafunzi hao kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo taulo za kike kwa wasichana.

No comments:

Post a Comment

Pages