Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), leo Juni Mosi,2022.
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a amesema maeneo mengi ya nchi yatakumbwa na vipindi vya upepo mkali huku hali ya joto ikitarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 4oC na 18oC.
Hali hiyo ni matokeo ya kipindi cha kipupwe kilichoanza Juni, Julai hadi Agosti (JJA), 2022 hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam leo Juni Mosi,2022. Dk. Chang’a amesema mwelekeo wa hali ya hewa kwa JJA inaonesha kuwepo kwa ukavu, baridi na upepo mkali kwenye maeneo mengi ya nchi.
Alisema kanda ya kusini Mkoa wa Ruvuma, hali ya baridi ya kawaida hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi kuwa kati ya nyuzi joto 6 oC na 14 oC.
Dk. Chang’a alisema hali hiyo kwa kanda ya Ziwa Victoria mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) inatarajiwa kuwa na joto la chini hadi juu ya kawaida kati ya nyuzi joto 14oC na 20oC katika maeneo mengi ya ukanda huo.
“Ukanda wa Pwani ya kaskazini mikoa ya (Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba) hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi.
“Kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 22oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani ni 18oC na 22oC katika maeneo ya nchi kavu.
“...Hata hivyo, maeneo yenye miinuko hususan katika mikoa ya Tanga na Morogoro yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 18oC,” amesema Dk. Chang’a.
Alibainisha kwamba Kanda ya nyanda za juu kaskazini mashariki mikoa ya (Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10oC na 18oC.
Hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 10 oC hasa kanda ya magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma),
hali ya baridi ya kawaida na joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14oC na 20oC.
Alisema Kanda ya kati mikoa ya Singida na Dodoma, hali ya baridi ya kawaida hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 12oC na 18oC.
Kwa mujibu wa Dk. Chang’a ukanda wa pwani ya kusini mikoa ya Mtwara na Lindi, hali ya baridi ya kawaida hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14oC na 22oC.
“Kanda ya nyanda za juu kusini-magharibi mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na maeneo ya kusini ya Mkoa wa Morogoro, hali ya baridi ya kawaida hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi kuwa kati ya nyuzi joto 4oC na 14 oC.
No comments:
Post a Comment