June 09, 2022

JK AONYA UKABILA

Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Prof. Rwekaza Mukandala (kulia), wakati akiwasili katika kongamano la 13 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, akitoa hotuba yake wakati akifungua kongamano la 13 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, linaloendelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

RAIS mstaafu wa awamu ya nne , Jakaya Kikwete amewataka vijana kuziishi falsafa za Nyerere kwa kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuepuka masuala ya ukabila.


Pia Kikwete amewataka vijana kupenda kusoma vitabu ili kujiongezea maarifa kwani hayapatikani kwa kuchati. 

Kikwete aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam katika kongamano la 13 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema katika vitu ambavyo Mwalimu Nyerere alifaulu ni kuondoa ukabila, udini na ukanda ambapo alihakikisha mambo hayo hayana nafasi, bali watu wanakuwa wamoja na kushirikiana.

"Ukabila vyuoni na sehemu zingine haufai...Nyerere alihakikisha anaondoa vitu vitu na asingefurahi kuona vinaibuka vyama vya ukabila, sijui mambo ya uchifu. Nchi inatakiwa kuendelea kuwa yenye usawa,  umoja na yenye amani," alisema Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha UDSM. 

Aliwataka vijana watambue ni zamu yao kuongoza Taifa  ili kuweza kulifikisha mbali zaidi katika uchumi wa juu pamoja na kujituma.

"Ukishafika chuo wewe ni mtu mzima, hivyo  unatakiwa kufanya majukumu yako ili kujenga Taifa. Changamoto kubwa iliyopo kwa vijana wa sasa hampendi kusoma vitabu, utakuta muda wote mtu ameinamia simu yake anachati.

"Kuna vitu vina faida na hasara zake lakini hakuna faida katika kuchati lakini ukisoma vitabu utajiongezea maarifa ambayo yatakusaidia katika mambo mbalimbali," alisema Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha UDSM," alisema Kikwete. 

Alisema, vijana wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na maono na wanaishi maisha ya uadilifu, kupendana, kufanya kazi kwa kujituma, kujitolea na hata kama ikibidi kujitoa muhanga.

"Kama ambavyo Mwalimu Nyerere alipoweka chaguo aache kazi au shughuli za vyama, lakini akachagua kuacha kazi pamoja na kwamba alikuwa ameoa ana watoto wadogo na anaishi Dar es Salaam sio kama ana shamba hapa lakini alikuwa tayari ili mradi aendeleze vita vya kumuondoa mkoloni ili taifa liweze kukomboka," alisema na kuongeza:

"Kwahiyo vijana wa sasa nao ni wakati wao, kuwa na mtazamo kama huo, sisi zamu yetu imeisha tunawaangalia nyie,".

Naye Mkurungezi Mtendaji wa Hakielimu John Kilage alisema miaka 100 ya maisha aliyoyaishi Hayati baba wa Taifa mwalimu Julias Nyerere yalijikita zaidi katika mkazo katika suala la elimu kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu na ujuzi.

Alisema zipo chagamoto zilizopo katika mfumo wa elimu hivyo ni muhimu kuzifanyia kazi ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

" Upo umuhimu wa kuboresha mfumo wa elimu licha kuwepo kwa chagamoto kwani Hayati baba wa Taifa mwalimu Julias Nyerere aliweka mkazo katika suala hili na kutokupoteza utambulisho wetu"alisema

Kwa upande Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es salaam Profesa William Anangisye alisema kongamano hilo litafanyika kwa siku tatu ambapo wadau mbalimbali wamealikwa kutoa mada zinazoyaenzia maisha yake.

Alisema chuo kikuu kimekuwa kikienzi fikra za hayati baba wa Taifa mwalimu Julias Nyerere kwa kuyafundisha yale yote .

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Rwekaza Mukandala alisema miaka ya nyuma walikuwa wanazungumzia sana siasa lakini safari hii wakaona wazungumzie suala la uchumi, kuongeza mitaji na suala la kujituma hasa kwa vijana.

"Ni dhahiri kabisa nchi imepitia katika kipindi kigumu cha uchumi ulioporomoka, kasi ya uchumi ilipungua kutoka asilimia 7 mpaka 4, lakini sasa hivi dalili ni nzuri pamoja na kwamba kuna vita hii ya Ukraine," alisema Mukandala. 


No comments:

Post a Comment

Pages