June 21, 2022

Naibu Waziri Khamis akagua uoteshaji miti Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akikagua ukuaji wa mti uliopandwa katika Barabara ya Ihumwa eneo la Shule ya St. Peter Claver wakati wa ziara ya kukagua zoezi la upandaji miti jijini Dodoma leo tarehe 19, Juni 2022.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akikagua miti katika eneo la Medeli wakati wa ziara ya kukagua zoezi la upandaji miti jijini Dodoma leo tarehe 19, Juni 2022. (PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS).

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis leo tarehe 19 Juni, 2022 ametembelea na kukagua zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma.

Akikagua zoezi hilo katika Barabara ya Ihumwa – Iyumbu, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Medeli, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Iyumbu, Mhe. Khamis ameonesha kuridhishwa na usimamizi na ufuatiliaji wa miti hiyo tangu ilipopandwa.

Alitoa pongezi kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Jiji la Dodoma, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na wadau mbalimbali wanaotoa mchango katika utunzaji wa miti.

“Leo tumefanya ziara ya kukagua miti ambayo imepandwa kwasababu kuu mbili moja ni Sera yetu ya Mazingira inatuelekeza tupande miti na kuiendeleza ili tujue ipi imeota na ipi imekufa, lakini pia tunafanya ziara hii kufuatia maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhhe. Dkt. Philip Mpango ambaye kwa nayakati mbalimbali amekuwa akitusisitiza kufuatilia miti inayopanadwa,” alisema.

Aidha, Naibu Waziri Khamis alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa mazingira kuwa na ushirikiano katika kuhakikisha miti inaoteshwa na kutunza ili kutimiza azma ya kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na hivyo kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

Pia aliwasihi Tanroads wawe wanawafuatilia watu waliowapa zabuni ya kumwagilia miti kuwa wafuatilie zoezi hilo kama linafanyika kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Maendeleo ya Rasilimali Misitu kutoka TFS, Bi. Patricia Manonga alisema Programu ya Dodoma ya Kijani wanatarajia kuongeza uzalishaji wa miche kutoka milioni moja hadi milioni mbili kwa mwaka kupitia kitalu kilichopo Mailimbili.

Alisema hadi kufikia sasa tayari TFS imezalisha miche zaidi ya milioni 57 ambayo imepandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma ambapo zoezi rasmi lilizinduliwa mwaka 2017.

Akitoa mchanganuo wa miti iliyopandwa, Bi. Patricia alifafanua kuwa katika eneo la Medeli ilipandwa miti 500, Iseni miti 1,200 na Iyumbu ilipandwa miti ya kivuli takriban 1,000 ambapo amezitaka taasisi kupanda miche wanayopatiwa badala ya kuiacha ikaharibika.

No comments:

Post a Comment

Pages