June 21, 2022

RC Malima awaangukia Handeni ongezeko bajeti ya dawa


Na Mwandishi Wetu


MKUU wa Mkoa (RC) wa Tanga, Adam Malima, amewataka wananchi wilayani Handeni kuwa na subira wakati serikali inafanya tathmini ya namna ya kuwapatia dawa za kutosheleza mahitaji yao katika hospitali ya wilaya hiyo.

RC Malima ametoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni, Baraza la Madiwani kwenye halmashauri hiyo kuomba serikali kuangalia namna ya kuwaongezea bajeti ya dawa kwani hospitali hiyo inahudumia watu wengi zaidi kuliko mahitaji ambapo kiuhalisia inakadiriwa kuhudumia wagonjwa 96,000 lakini kutokana na jiografia ya wilaya hiyo inahudumia takribani wagonjwa 456,000.

“Hatuwezi kupata mabadiliko kwa sasa hadi Hospitali ya Handeni ianze kufanya kazi na kasha tufanye tathmini ya mizania kujua baada ya hospitali ile kupatikana kiuhalisia bado watu wanagapi wanakuja hapo, kisha tutalipatia ufumbuzi suala hilo ili wananchi wetu waweze kupoata huduma stahiki,” amesema Malima akijibu hoja hiyo.

Pamoja na mambo mengine. RC Malima amewataka madiwani hao kusimamia fedha za miradi ya maendeleo na kuleta maendeleo kusudiwa katika maeneo yao.

Awali akitoa hoja yake hiyo kwenye kikao cha kupitia na kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika halmashauri hiyo, Mkombati amesema hoja yake hiyo inatokana na ukweli kwamba jiografia ya wilaya hiyo fedha za dawa zinakuja zikiwa tayari ni bajeti ya watu 96,000 wanaotakiwa kuhudumiwa lakini ongezeko la watu 456,000 linasababisha watu kutopata huduma stahiki na malalamiko kuwa mengi.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunaomba utusadie kwa jiografia kwa baadhi ya maeneo kwa mfano Kata ya Kang’ata hata tukiwa na hospitali kubwa kiasi gani kule Mkata au Kilindi bado wataendelea kuja kwetu.

“Madaktari wetu wanajitahidi sana lakini dawa zinazokuja zimebajetiwa kwa watu hao 96,000 pekee ni wazi kuwa hospitali inaelemewa na mwisho wa siku malalamiko yanakuwa makubwa lakini changamoto kubwa inakuwa ni hiyo kwa hiyo, kwa nafasi yako naamini utatusaidia ili tuweze kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wetu wa Handeni,” amesema Mkombati.

Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imefanikiwa kupunguza hoja za ukaguzi kutoka 56 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia hoja 33 mwaka 2021/22.

No comments:

Post a Comment

Pages