June 05, 2022

SERIKALI YA TANZANIA YAPONGEZWA KUIBEBA AJENDA YA MAZINGIRA


Mratibu wa Shirika  la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UN Environment),Tanzania Clara Makuya wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu wiki ya Mazingira katika maonyesho  yanayoendelea kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

SHIRIKA la mazingira la Umoja wa Mataifa (UN Environment), Tanzania limeipongeza Serikali ya Tanzania  kuibeba ajenda ya utunzaji mazingira kwa uzito mkubwa kwa kuwa ni moja ya mafanikio katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku likieleza changamoto ya ongezeko la idadi ya watu ikilinganishwa na ukubwa Ardhi iliyopo.

Ardhi iliyopo toka Uhuru Mwaka  1961hadi sasa Mwaka 2022 ni ileile skwea mita 945,000 ambapo idadi ya watu imeongezeka zaidi ya mara sita toka watu milioni Tisa hadi kufikia zaidi ya milioni60.

Hayo yameelezwa Juni 4,2022 Jijini  Dodoma na Mratibu wa Shirika hilo,Clara Makuya wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu wiki ya Mazingira katika maonyesho  yanayoendelea kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete.

"Tumeona namna Serikali ambavyo imekuwa ikitoa kipaumbele katika suala zima la kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi katika hatua  ya Viongozi wa juu wa Serikali kwa watunga Sera hadi kufikia mtu mmoja mmoja wamekuwa na muamko  kuhusu suala zima la utunzaji wa mazingira", amesema

Sambamba na hilo amebainisha  kuwa Sera zote nchini Tanzania zimekuwa zikiangalia eneo la mazingira hivyo katika suala la utunzaji mazingira limezingatiwa ikiwa ni pamoja na Kushirikisha sekta binafsi.

"Sisi kama Umoja wa Mataifa  tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania na kuipongeza kwa hatua yakuibeba ajenda ya mazingira kama ilivyo kuwa ajenda ya ukimwi kwani ni moja ya mafanikio makubwa katika utunzaji amazingira,"amesema

Akizungumzia changamoto ya Rasilimali ameeleza kuwa ukubwa wa eneo la nchi ni dogo tangu Uhuru halijaongezeka lakini idadi ya watu imekuwa ikiongezeka na mwisho wa siku Rasilimali walizonazo hazitoshi hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Kimataifa la UNDCF Aine Mushi ameeleza kuwa  wanawakilisha mataifa mengine na kwamba wanaisaidia Serikali katika kuzuia mabadiliko ya athari za tabia Nchi hivyo wamekuja na Nishati mbadala katika kuwawezesha wananchi kutumia Nishati hizo.

Mushi ameeleza kuwa lengo la Mradi huo wa Nishati mbadala ni Kuisaidia Serikali kupunguza athari za mabadiliko ya tabia Nchi.

"Tumekuwa tukiihamasisha Serikali kuwawezesha wananchi kutumia Nishati mbadala ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi na  tayari tumeshawafikia wananchi wa Wilaya za Chamwino,Kondoa na Mpwapwa zilizopo Mkoani Dodoma na Mradi huu tumeanza na Mikoa mitano ikiwemo Dodoma,Dar -es-Salaam,Mwanza na Pwani," amesema.

Mratibu huyo ameongeza kuwa  wamekuwa wakifanya kazi na Ofisi ya Makamu wa Rais na Halmashauri na kuzishawishi katika kupanga bajeti ya mazingira pamoja na kutunga Sera ambazo zinatekelezeka.

Emilian Masanja  toka Wizara ya Nishati,amesema kuwa  katika mipango ya Serikali nikuhakikisha wananchi wanaondokana na matumizi  ya Nishati ambazo zina madhara.

Masanja ameongeza kuwa Wizara ya Nishati kwakushirikiana na Wadau wa maendeleo kupitia Mradi huo wa Nishati mbadala wamejipanga kuzishirikisha sekta binafsi Katika uendelwzaji wa teknolojia za kupikia.

No comments:

Post a Comment

Pages