July 14, 2022

Mbunge Lugangira awasilisha ujumbe mzito Kikosi Kazi

 


Neema Lugangira Mbunge wa Viti Maalum (CCM) akiwasilisha maoni na mapendekezo ya kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini mbele ya wajumbe wa Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Na Selemani Msuya

 

MBUNGE wa Viti Maalum CCM, Neema Lugangira ameshauri Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi kupitiwa upya ili kuleta usawa wa kijinsia.

Lugangira amesema hayo jana baada ya kutoa maoni kwa Kikosi Kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan kinachoshughulikia masuala ya demokrasia yaliyoibuliwa kwenye kikao cha wadau kilichofanyika Disemba 15 hadi 17 mwaka jana, jijini Dodoma.

Alisema amelazimika kuwasilisha maoni hayo katika eneo namba nne la kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa kutokana na ukweli kuwa kuna ombwe kubwa.

Mbunge huyo alisema amekiambia kikosi kazi kuhusu changamoto zilizopo kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi ili ziweze kufanyiwa marekebisho na kuendana na wakati wa sasa.

“Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi ni muhimu sana katika kufanikisha lengo la usawa ila kwa sasa haina meno. Mfano Sheria ya Vyama vya Siasa haimpi meno Msajili kufuatilia uwepo wa asilimia fulani ya wanawake ndani ya vyama, hivyo kinachotokea ni utashi wa vyama pekee,” alisema.

Mbunge huyo alisema iwapo Sheria itampa meno Msajili anaweza kuhoji pale ambapo vyama vitashindwa kutekeleza dhana ya usawa wa kijinsia.

Alisema Katiba inaelekeza uwakilishi wa wanawake ni asilimia 30 ya wabunge wa viti maalum lakini sheria ipo kimya jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa kina na sheria kuweka kiwango mahususi.

Lugangira alitolea mfano katika Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kuwa uwakilishi wa wanawake ni asilimia 2 hali ambayo inaonesha wanawake bado ni wachache.

Kuhusu Sheria ya Uchaguzi mbunge huyo alisema ni wakati muafaka wa kutambulika makosa ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake.

“Sheria ya Uchaguzi iliyopo haitambui makosa ya ukatili wa kijinsia kama moja ya makosa ambayo mgombea anaweza kupinga mgombea mwenzake, haya yote yanahitaji kuangaliwa upya,” alisema.

Alisema pia Sheria hiyo haijafafanua ni namna gani mgomnea akitolewa lugha za kuejeli anaweza kuwasilisha, lakini pia mchakato wa kusikiliza huwa unachukua muda mrefu.

Lugangira alishauri pia uundwaji wa kamati za maadili kuzingatia jinsia ili kuwawezesha wanawake kusikilizwa  na watu ambao wanahisi kilichofanyika.

Akizungumzia dhana ya kuwa wanawake hawapendani na kwamba ndio sababu ya wao kushindwa kushinda katika chaguzi mbalimbali Lugangira alisema hoja hiyo imekuwa ikitumiwa na wanaume katika kuwadidimiza.

Alisema iwapo maoni ambayo wanatoa kwenye kamati yatafanyiwa kazi vizuri ni wazi kuwa usawa katika uwakilishi kwenye siasa utapatikana.


No comments:

Post a Comment

Pages