July 29, 2022

Taarifa za Tasaf kutumika mikopo elimu ya juu



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza wakati wa Mkutano na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam leo Julai 29, 2022. NA MPIGA PICHA WETU. 

Baadhi ya Wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo .

 

Na Irene Mark


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema taarifa sahihi za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), zinatambulika na zinamsaidia mwanafunzi kupata mkopo wa elimu ya juu.

Akizungumza wakati wa mkutano kati ya Waziri Profesa Mkenda, wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam, leo Julai 29, 2022 amesema utaratibu wa kupata mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu umeboreshwa.  

Amesema serikali imetenga sh.bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu huku akiwataka waombaji wafuate taratibu zilizowekwa na kutoa taarifa sahihi.

“Kila mwenye sifa atapata mkopo nawahakikishia mikopo hii itatolewa kwa haki kwa wote wenye vigezo vya kupata mkopo huo.

“Changamoto ya kutoa mikopo ni kubwa na tunakwama kutokana na taarifa za waombaji ndio maana tunasisitiza zitolewe taarifa sahihi,” amesema Profesa Mkenda.

Katika kukabiliana na changamoto hizo Profesa Mkenda ameunda timu maalum ya wataalam watatu itakayosaidia uhakiki wa taarifa za waombaji kidijitali.

Profesa Mkenda amesema timu hiyo inaundwa na Allan Mushi, Iddi Makame kutoka Zanzibar na Dk. Martin Chegere wataosaidia uhakiki wa taarifa za waombaji kwa njia za kiteknolojia.

Amewataka wananchi wanaowajua waombaji wasio na sifa za kupata mkopo wa elimu ya juu kutoa taarifa kwa mamlaka husika huku akiwahakikishia ulinzi na kuwashughulikia wadanganyifu hao.


No comments:

Post a Comment

Pages