July 08, 2022

TCU yafungua Dirisha la waombaji Shahada ya Kwanza Taasisi za Elimu ya Juu 2022/2023

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 8, 2022 wakati wa kutangaza kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza.

 

Na Mwandishi Wetu

 

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufungua Dirisha la waombaji wa Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. 


Akitangaza kufunguliwa kwa dirisha hilo Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, amesema kuwa kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita, Tume imefungua dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza kuanzia leo Julai 8, 2022 badala ya Julai 15, 2022 iliyokuwa imepangwa awali, Dirisha hilo litakuwa wazi hadi Agosti 5, 2022.

"Kufunguliwa mapema kwa dirisha hilo kunatokana na kutangazwa kwa matokeo ya mitihani ya kidato cha sita hivyo basi dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia Julai 8, 2022 hadi Agosti 5, 2022”.  alisema Prof. Kihampa.

 

Prof. Kihampa aliongeza kuwa utaratibu wa Kutuma Maombi ya Udahili yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo muombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda. Mwongozo wa programu zilizoidhinishwa kudahili na vigezo stahiki (Undergraduate Admission Guidebooks for 2022/2023) unapatikana kwenye tovuti TCU www.tcu.go.tz  

 

"Tume inawahimiza waombaji wa udahili kuendelea kupata sahihi kupitia tovuti ya TCU www.tcu.go.tz, tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza." alisema Prof. Kihampa".

Aidha Tume hiyo imewataka waombaji wa udahili na wananchi kuhudhuria Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo watapata fursa ya kuonana ana kwa ana na Vyuo vya Elimu ya Juu, Maonesho hayo yatafanyika kuanzia Julai 18 hadi Julai 23, 2022.  

No comments:

Post a Comment

Pages